You are currently viewing Wenyeviti wa mitaa waridhishwa na uwekezaji sekta ya maji Temeke

Wenyeviti wa mitaa waridhishwa na uwekezaji sekta ya maji Temeke

Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Temeke wamepongeza na kuridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika uboreshaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi katika Wilaya hiyo.

Hayo yamebainishwa katika ziara inayoendelea kwa siku ya pili ya Wenyeviti wa Serikali za mitaa kwenye vyanzo na miradi ya DAWASA inayolenga kujenga uelewa wa pamoja wa utoaji wa huduma ya Maji kwa Viongozi pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kulinda miundombinu ya maji.

Awali kabla ya ziara kwenye Mtambo wa kuzalisha maji Mtoni uliopo Wilayan Temeke, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire aliwashukuru viongozi hao kwa muitikkl mkubwa na kushiriki ziara  hiyo itakayosaidia kuongeza tija ya utendaji kwa Mamlaka na kwa wananchi pia.

“DAWASA tuna amini huduma endelevu ni ushirikishwaji wa watu na wenye watu ni nyinyi Wenyekiti wa Serikali za Mitaa, tunaamini katika kushirikiana ili kuimarisha huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika maeneo yenu ya Wilaya ya Temeke,” alisema Mhandisi Bwire.

Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti katika Wilaya Temeke Ndugu Sharifu Jumbe ameipongeza DAWASA nakubainisha kuwa ni jambo la historia katika Wilaya ya Temeke kwa viongozi wa mitaa kupewa fursa ya ushirikishwaji katika mikakati mbalimbali kuboresha huduma za Maji kwa wananchi.

“Kwanza tunaishukuru DAWASA kwa kutambua umuhimu wa Viongozi wa Serikali za mitaa, kupitia ziara hii tumeridhika na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika utekelezaji wa miradi yao,” amesema. 

“Pili tumejifunza mengi kuanzia utoaji wa huduma za Majisafu na Usafi wa Mazingira, hivyo tutasimamia vilivyo utoaji wa huduma kwa wananchi na kutoa ushirikiano wa kutosh kwa DAWASA ili lengo litimie,” aliongeza  Ndugu Jumbe. 

Ziara hiyo iliyoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji Maji DAWASA, Mhandisi Tyson Mkindi, ilianzia katika mradi wa Usafi wa Mazingira Vikunai Kata ya Kijichi ukiwa ni sehemu ya mradi wa kimkakati unaohusisha ujenzi wa vituo nane vya huduma kwa Umma unaotekelezwa katika Wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam utakaosaidia kupunguza adha ya uchafuzi wa Mazingira lakini utasaidia kuzalisha gesi pamoja na kupata mbolea kwa shughuli za kilimo ambao umetekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 16.

Vilevile viongozi hao walitembelea Mtambo wa uzalishaji maji Mtoni ambao unahudumia kwa kiwango kikubwa Wakazi wa Wilaya Temeke na kuonesha hatua zote za kutibu maji hadi kumfikia mtumiaji na pia kutembelea Kisima cha Maji Makangarawe ikiwa ni sehemu ya kisima kati ya visima 31 vilivyopo na vinavyohudumia Wilaya Temeke.

Mamlaka inaendelea na ziara na mafunzo ua ushirikishwaji wa Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Wilaya zote Tisa za kihuduma katika Mikoa ya Dar es salaam na Pwani.

Leave a Reply