You are currently viewing Waziri Mkuu aridhishwa ujenzi sekondari Mwanza girls, aweka jiwe la msingi
Shule ya Sekondari Mwanza Girls

Waziri Mkuu aridhishwa ujenzi sekondari Mwanza girls, aweka jiwe la msingi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Mwanza (Mwanza Girls’) na kuweka jiwe la msingi la msingi la shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Ihushi, kata ya Bujashi, wilayani Magu.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule za sekondari za bweni 26 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 ambazo zinaendelea kujengwa nchi nzima kwa ajili ya wasichana wanaosoma masomo ya sayansi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Akizungumza na wananchi waliofika shuleni hapo leo (Jumamosi, Desemba 21, 2024), Waziri Mkuu amesema suala la elimu ni hitaji la muhimu kwa ajili ya watoto wa Kitanzania na kwamba ujenzi wa shule hiyo chini ya mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais alielekeza tutekeleze miradi inayogusa moja kwa moja ya kila siku ya wananchi. Shule ni hii inaribia kukamilika; katika sekta ya afya zililetwa sh. milioni 250 kwa ajili ya zahanati tano; Hospitali ya Wilaya tayari imekamilika, hivi karibuni sh. milioni 700 zililetwa kukamilisha majengo ikiwemo wodi ya wanaume.”

Amesema kwenye umeme, vijiji 81 kati ya 82 vya wilaya hii tayari vimepata umeme na kijiji kimoja kilichobakia kiko kwenye kisiwa ndani ya Ziwa Victoria lakini tayari mikataba imeshainiwa ili maeneo ya visiwani yaweze kupelekewa umeme.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani amesema ujenzi wa shule hiyo ambayo iko kwenye hatua za umaliziaji, umegharimu sh. bilioni 4.5 na kwamba hadi sasa wanafunzi 514 wamekwishaanza masomo kwenye shule hiyo.

Naye, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba alisema ifikapo Januari 2025, shule hiyo inatarajiwa kupokea wanafunzi 120 wa kidato cha kwanza.

Leave a Reply