You are currently viewing Waziri mkuu akagua maendeleo ya mradi wa maji Bujora – Kisesa wilayani Magu

Waziri mkuu akagua maendeleo ya mradi wa maji Bujora – Kisesa wilayani Magu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana Desemba 21, 2024 amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa tenki la kuhifadhi maji la Bujora – Kisesa lililoyopo wilayani Magu mkoani Mwanza ikiwa ni mpango wa muda wa kati wa kuboresha huduma ya maji Mwanza ambao unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.54.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (France Development Agency) hadi kukamilika kwake na mpaka sasa umefikia asilimia 93 na unatarajiwa kuhudumia wananchi 75,000 wa maeneo ya maeneo ya Kisesa, Bujora, Igudija na sehemu za jirani.

Akizungumza na wananchi wa eneo la Bujora baada ya kukagua mradi huo Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi mikubwa inayowagusa wananchi moja kwa moja kwenye sekta za elimu, afya, maji, kilimo, uvuvi na barabara.

Kwa Upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara hiyo itaendelea kusimamia maagizo ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata maji katika maeneo yao.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alisema hataki kuona wananchi wanateseka kutafuta maji,” amesema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Nelly Msuya amesema kuwa Matenki mengine yatajengwa katika maeneo ya vilima vinavyozunguka Mji wa Mwanza ikiwemo Nyamazobe (lita milioni 10), Buhongwa (Lita milioni 5), Fumagila (Lita milioni 10) na Usagara (lita milioni 1).

“Utekelezaji wa mradi huu wa thamani ya Tsh. Bilioni 49 umeanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili (2) ifikapo Desemba 2026,” amesema.

Aidha, amesema kuwa ujenzi wa tenki la Bujora – Kisesa lenye ujazo wa lita milioni 5, unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari, 2025.

Leave a Reply