Na Mwandishi Wetu, Arusha
Watumishi 65 wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), jana Februari 7, 2025, wamefanya ziara ya kihistoria ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kwa ajili ya kushuhudia vivutio mbalimbali vya utalii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Bakari George, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru amesema ziana hiyo imelenga kutoa hamasa ya utalii wa ndani kwa watumishi wa chuo hicho sambamba na kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kutangaza na kukuza sekta ya utalii nchini.

Dkt. Bakari amesisitiza kuwa ziara hiyo imewapa fursa watumishi wa TICD kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro ikiwemo wanyama wakubwa watano (Big 5) Simba, Tembo, Faru, nyati na Chui wakiwa katika mazingira ya asili yaliyohifadhiwa vizuri.
Bi. Patricia Kabaka na Bw.Noeli Mkwizu, miongoni mwa watumishi walioshiriki ziara hiyo wameushukuru uongozi wa Chuo kwa juhudi kubwa inazofanya kwa watumishi hao ambapo wameitaja ziara hiyo kuwa itakwenda kuongeza tija na hamasa katika utendaji wa majukumu yao lakini pia kuhamasisha watumishi wengi zaidi kutembelea hifadhi hiyo wakiwa na familia zao.