You are currently viewing Watia nia ubunge 55 waitikisa Chadema, wapinga kuzuia uchaguzi

Watia nia ubunge 55 waitikisa Chadema, wapinga kuzuia uchaguzi

Watia nia wa Ubunge 55, kwenye uchaguzi wa 2025, kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo wametoa sababu tisa za kupinga mpango wa Chama hicho kuzuia uchaguzi, katika waraka waliwandikia Katibu Mkuu.

Watia nia 55 wa ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mwaka 2025, wakiwakilisha zaidi ya 200 walioonesha nia, akiwemo baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho, wameibuka na hoja tisa kuhusu msimamo wa chama huo wa kutoshiriki uchaguzi endapo hakutakuwa na mageuzi ya kisiasa (‘No reforms, no election’).

Kupitia waraka walioutuma Aprili 4, 2025 kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, watia nia hao wameeleza kuwa msimamo huo kwa sasa unakinzana na malengo yake ya awali. Wamedai kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya mchakato huo, wakisema hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama kitendo cha jinai.

Kwa mujibu wa waraka huo, njia pekee ya kuzuia uchaguzi usiyo huru ni kushiriki mchakato huo kwa kuingiza wagombea, ambao wanaweza kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika maeneo mahsusi yenye viashiria vya hujuma, badala ya kuwa nje ya mchakato mzima.

Katika sababu hizo wameeleza kuwa, “Tunaona kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya uchaguzi.”

“Dhana ya “No Reforms, No Elections”, ilianza kama kampeni mnamo mwezi Januari mwaka 2020 baada ya “retreat” ya Kamati Kuu iliyofanyika Makueni, nchini Kenya, na haikuwa na tafsiri ya kuzuia uchaguzi bali ilikuwa inalenga kuhamasisha uungwaji mkono.”

Sababu ya tatu : Kwa muda mfupi uliosalia, hatuoni uwezekano wa kutekeleza kwa ufanisi mkakati wowote madhubuti wa kuzuia uchaguzi. Tayari, uchaguzi wenyewe umeshaanza kupitia zoezi la uandikishaji wapiga kura ambalo limeshafanyika kwenye mikoa mingi nchini na mchakato wa uchaguzi unaendelea kwa hatua ya mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.

Sababu ya nne : “Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, ibara ya 4 inayohusu madhumuni ya Chama, dhumuni kuu la Chama ni kuongoza dola na kutekeleza madhumuni mahsusi ya kisiasa kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4.1, madhumuni ya kiuchumi yaliyopo kwenye kifungu 4.2 pamoja na madhumuni ya kijamii kama yalivyoainishwa katika kifungu 4.3. Kwa hiyo, kushiriki uchaguzi ili kuongoza dola ni sharti la kimsingi la kikatiba.”

Sababu ya tano : Ibara ya 5.2.2 ya Katiba ya Chama imetamka haki ya mwanachama wa CHADEMA kuwa ni pamoja na kuchaguliwa kuongoza na kuwakilisha Chama katika ngazi yoyote kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa ya sifa za uongozi. Mpango wa kuzuia uchaguzi unaweza kukosa uhalali wa kutosha kikatiba kwa kuathiri haki za wanachama wa CHADEMA wanaotaka kugombea. 

Sababu ya Sita : Ukiondoa chama chetu, mpaka sasa hakuna chama kingine hata kimoja cha siasa kinachounga mkono mpango wa kuzuia uchaguzi ikiwa reforms hazitopatikana. Kinyume 

chake, kuna Chama kimoja tu cha upinzani ambacho kinapigania “reforms” lakini huku kikiendelea kujipanga kushiriki uchaguzi. Vyama vingine hususani vile vyenye kawaida ya kutumika na CCM, vimeendelea kutangaza nia zao za kushiriki uchaguzi.

Sababu ya Saba : Viongozi wa dini na madhehebu yenye waumini wengi hapa nchini, tayari wamehimiza na wanaendelea kuelimisha na kuhamasisha waumini wao kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwaajili ya kushiriki uchaguzi. Hali hii inaashiria kuwa ni ama Chama chetu kimechelewa au tayari kimekwama kupata uungwaji mkono wa wadau 

muhimu katika mpango wa kuepuka uchaguzi usio na reforms. 

Sababu ya Nane : Uchunguzi na uchambuzi wetu unaonesha kuwa wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai yetu ya “reforms”, lakini wanasita kuunga mkono mpango kamili wa Chama chetu wa kuzuia uchaguzi iwapo “reforms” hazitopatikana, kwani hali hiyo kwao inatafsiriwa kuwa ni karibu sawa na kufanya uasi au kuvunja katiba na sheria zilizopo licha ya ubaya wake. Kwa maneno mengine, msisitizo wa kuzuia uchaguzi unaathiri au kupunguza kasi ya uungwaji mkono katika madai ya msingi ya reforms.

Sababu ya Tisa : Kushindwa kuzuia uchaguzi katika dakika za mwisho (ikiwa jitihada za kupata reforms zitakwama), kunamaanisha kuwa Chama hakitokuwa tena na muda wa kujiandaa na hivyo hakitoshiriki kabisa uchaguzi huo.

Waraka huo umesainiwa na wanachama 55, wakiwemo Catherin Ruge, Julius Mwita, Suzan Kiwanga, Grace Kiwelu, Henry Kilewo, Patrick Assenga, Lembrus Mchome, Vitus Nkuna, Wakili John Mallya.

Leave a Reply