You are currently viewing Wanajeshi 2 JWTZ wapoteza maisha Kongo, 4 wajeruhiwa

Wanajeshi 2 JWTZ wapoteza maisha Kongo, 4 wajeruhiwa

WANAJESHI wawili wa Jeshi la linzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoshiriki shughuli za Ulinzi wa Amani chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) nchini Kongo wamefariki.

Pia wanajeshi wanne wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya SAKE na GOMA yaliyofanywa na Waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari 2025.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Kanali Gaudentius Gervas Ilonda imesema JWTZ limewapoteza Askari wake idadi wawili (02) na wengine idadi wanne (04) kujeruhiwa. 

“Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma. Taratibu za kuisafirisha mili ya Marehemu wetu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC. Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka majeruhi wetu na aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi, Amina,” imesema taarifa hiyo na kuongeza;

“Aidha, vikundi vyetu vilivyopo nchini DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya Uongozi wa SADC.”

JWTZ limeshiriki kulinda Amani katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na nchini Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aidha, katika ushiriki wake, JWTZ linaendelea kulinda amani kwa Mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika huko Mashariki mwa nchi ya DRC (SAMDRC) eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulizi kati ya Waasi wa M23 wanaopambana na Jeshi la DRC (FARDC) katika maeneo hayo.

Leave a Reply