Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), William Lukuvi ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya kusini maarufu kama Bangulo.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika mapema Desemba 2024, utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 katika kata za Pugu station, Kipinguni, Kiluvya, Kitunda, Mzinga, Kinyerezi na Msigani.
“Siku za Nyuma nikiwa mkuu wa mkoa maeneo haya ya Bangulo na maeneo jirani yalikuwa na shida kubwa ya maji, nina furaha kuona inakwenda kumalizika kupitia mradi huu, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kutoa fedha za mradi mikubwa kama huu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora” ameeleza Lukuvi alipotembelea mradi huo jana tarehe 10 Oktoba, 2024.
Aidha, Lukuvi amemsisitizia Mkandarasi Kampuni ya M/S SINOHYDRO-STECOL JV kukamilisha kazi ili ukamilike kwa wakati na Wananchu waanze mwaka mpya 2025 na huduma ya majisafi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA ambaye ni Mkurugenzi wa mipango na tathmini, ndugu Paul Sulley amemuhakikishia Waziri Lukuvi kuwa mradi huo utamalizika kwa wakati katika muda uliopangwa na kunufaisha wananchi wa Majimbo matatu ya uchaguzi katika mkoa wa Dar es salaam.
“DAWASA imejidhatiti katika kukamilisha mradi huu na ifikapo Disemba 2024 ili wananchi wapate huduma, tumepokea maelekezo ya kufanya kazi usiku na mchana na tutamuelekeza mkandarasi kukamilisha kazi kwa wakati” alisema Sulley
Mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya kusini unagharimu kiasi cha Sh bilioni 36 na unajumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita Milioni 6 na ulazaji wa bomba kuu la usambazaji maji kwa umbali kilomita 119.