Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema kuwa mchakato wa kutengeneza rasimu ya Sera ya kuwawezesha wazawa (Local Content) kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kupitia sekta mbalimbali mtambuka utasaidia kujenga uchumi wa nchi pindi utakapokamilika.
Akizungumza wakati wa Kikao cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonaz amesema kuwa ili kuleta utekelezaji jumuishi kwa sekta zote za umma na binafsi, kuna umuhimu wa kutungwa kwa sera ya kitaifa ili kutoa fursa zaidi kwa Watanzania kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi.
“Malengo ya sera hii, pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushiriki wa Watanzania na taasisi za Kitanzania kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi kama inavyopendekezwa na wadau” amesema Dk. Yonaz ambaye ndiye Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho.
Amesema kuwa kupitia sera hiyo, Serikali inakusudia kufanya maboresho ya kuimarisha mifumo na sheria, ili Watanzania wawe na mazingira wezeshi ya ushindani katika soko la biashara.
Aidha, alisema kuwa lengo la utungaji wa sera hiyo ni kuwezesha mifumo mbalimbali ya utendaji Serikalini kusomana kwa njia ya kidijitali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
“Tanzania inaenda kuwa na mazingira bora ya ufanyaji kupitia ujio wa sera hii ya taifa,” alisema.
Mapendekezo hayo ya kamati ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mwenyekiti wa TNBC, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Juni mwaka huu .
Awali, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk. Godwill Wanga alisema kuwa katika kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara hapa nchini, sera hiyo itawasaidia Wafanyabishara wazawa kuwa na ushindi katika masoko ya ndani na nje.
“Hii ni hatua kubwa na bado tunaendelea na mchakato wa kuunganisha mifumo mingine, ukiwemo wa sekta binafsi ambayo bado haisomani,”amesema.
Katika kikao kazi hicho, washiriki wamesema kuwa uwepo wa sera hiyo utasaidia wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi na kuwezesha kutambulika kwa sekta isiyo rasmi ili nayo kwa ukamilifu ishiriki katika uchumi wa nchi.
Mmoja wa wajumbe, Henry Kimambo kutoka sekta ya Utalii alisema kuwa kumekuwa na migongano ya kiutendaji kwa baadhi ya taasisi, huku utitiri wa tozo mbalimbali wakati mwingine hukatisha tamaa watu kufanya biashara, lakini sera hiyo itaondoa changamoto hizo.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake, Mercy Sila, ameipongeza TNBC kuzileta pamoja sekta Binafsi na Umma kujadili rasimu ya sera hiyo itakayoweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa Watanzania.
“Hii itasaidia hasa makundi maalum ya wanawake na watu wenye ulemavu kuwa na mazingira mazuri ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi,” alisema Mercy.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mwenza wa Kamati au kikundi kazi anayetoka Sekta Binafsi, Vicent Minja amesifu hatua ya utungwaji wa sera hiyo na kuwa shirikishi kwa wadau.