Shughuli za upandaji wa miti zinaendelea TFS – Shamba la Miti Sao Hill kwa wahifadhi kuendelea kusimamia zoezi la upandaji wa miti ambalo linafanyika katika kipindi hiki cha masika.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha Kamati ya Ufundi ya Shamba kilichofanyika tarehe 7 Februari, 2025 ambacho hufanyika kila mwezi kwa ajili ya kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mpango kazi wa shamba kwa kipindi husika.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Mhifadhi Mkuu wa Shamba PCO Tebby Yoram, amewakumbusha na kuwataka wahifadhi wote kuendelea kusimamia shughuli zote za shamba ambazo zinaendelea kwa sasa na kuwa wabunifu zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ili kufikia malengo ya Shamba na taasisi kwa ujumla.
Amesema kuwa kwa sasa shughuli kubwa inayoendelea ni upandaji wa miti na zoezi hili linaendelea vizuri kutokana na maandalizi mazuri ya mashamba, uzalishaji wa miche na uwepo wa vitendea kazi kama vile magari ya kubeba miche yaliyotoka katika vituo vingine vinavyosimamiwa na TFS.
Vilevile, amepongeza ushirikiano uliopo ndani ya TFS kwani msaada wa vitendea kazi hasa magari kutoka shamba la miti Mbizi, shamba la miti Kiwira, Kanda ya Magharibi – Shinyanga, Kanda ya Kati – Dodoma na Kituo cha Mbegu Morogoro vimesaidia zoezi la upandaji kufanyika kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.
Naye Mhifadhi anayesimamia Uendelezaji wa Msitu SCO Said Singano amesema kuwa eneo linalotakiwa kupandwa miti kwa msimu huu wa mwaka 2024/2025 ni takribani hekta 4000 na hadi sasa jumla ya hekta 3291 zimeshapandwa miti na hivyo kufanya zoezi hili la upandaji kufanyika kwa wakati.
Amesema kuwa Shamba limepokea jumla ya miche 7,000 ya miti ya asili ambayo ni Mkangazi na Mkongo kwaajili ya kuipanda katika maeneo ya Misitu ya Asili ambayo yanapatikana ndani ya Shamba la Miti Sao Hill.
Aidha, mada mbalimbali zimejadiliwa katika kikao hicho ikiwemo tathmini ya mwenendo wa uvunaji na ukusanyaji wa maduhuli kuanzia mwezi Julai hadi sasa kutoka vyanzo mbalimbali kama vile uvunaji wa miti na utomvu, ufugaji nyuki na Utalii Ikolojia.
Shughuli nyingine ni pamoja na kupokea na kupitia yaliyojili katika zoezi la ukaguzi wa kazi katika robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ili kuona mwenendo wa shughuli hizo na kubaini changamoto zilipo ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka na kupokea taarifa ya rasimu ya mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2025/2026