You are currently viewing UNOC yaridhishwa na kasi ya mradi wa EACOP Tanzania

UNOC yaridhishwa na kasi ya mradi wa EACOP Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Tanga

SHIRIKA la Mafuta la Uganda (UNOC) ambalo ni mmoja wa wabia wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa upande wa Uganda, limeelezea kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa Tanzania baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo yake hapa nchini.

UNOC, kupitia Serikali ya Uganda inamiliki asilimia 15 ya mradi huo wakati Shirika la Maendeleo ya Mafuta hapa nchini  (TPDC) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania linamiliki pia idadi hiyo hiyo ya hisa.

Wanahisa wengine wa mradi huu unaoanzia Hoima nchini Uganda hadi Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga ni TotalEnergies yenye asilimia 62 na Shirika la mafuta nchini China (CNOOC) linalomiliki asilimia nane tu. 

Akizungumza wakati wa ziara yao katika kituo cha kuhifadhia mafuta kilichopo Chongoleani, Mwenyekiti wa Bodi ya UNOC Mathias Katamba amesema wameamua kufanya ziara hiyo kujionea namna utekelezaji wa mradi huo unavyoendelea kwa upande wa Tanzania kama sehemu ya ufuatiliaji.

“Tumetembelea maeneo mbalimbali ikiwemo sehemu ya baharini panapojengwa maegesho ya meli za kubebea mafuta kwa ajili ya kusafirishwa kwenda soko la kimataifa na pia tumetembelea eneo panapojengwa matenki makubwa manne ya kuhifadhia mafuta ghafi  yatakayotoka Uganda.

“Tukiwa kama wanahisa wa mradi huu, tumefurashiwa na hatua kubwa ya maendeleo ya mradi huu baada ya kujionea kazi mbalimbali zikiendelea kupitia wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi,” amesema.

Amesema kwa upande wa Uganda, ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini humo pia unaendelea, ambapo kazi ya kufukia mabomba yatakayosafirisha mafuta hayo ghafi kuja Tanzania kupitia mikoa mbalimbali tayari imeshaanza.

“Sisi Uganda na Tanzania kupitia idara zetu mbalimbali tunashirikiana kwa karibu sana katika kuhakikisha hakuna kinachokwamisha mradi huu ikiwemo viongozi mbalimbali wa nchi hizi kutembelea maeneo ya ujenzi ili kufuatilia maendeleo yake.” amesema.

Ameongeza kuwa mradi huu utakuwa na tija sana kiuchumi kwa faida ya nchi hizi mbili na watu wake kutokana na fursa mbalimbali ikiwemo ajira.

“Kuna baadhi ya watu wanaubeza mradi huu huu na kusema kuwa una athari kimazingira.

“Lakini sisi kupitia wataalamu wetu tulifanya tathmini ya maeneo mengi ya utekelezaji wake, ikiwemo tathmini ya upande wa mazingira na ulipaji mzuri wa fidia kwa watu wetu walioguswa kwa kuzingatia matakwa ya mashirika ya kimataifa,” amesema.

Naye Peter Mulisa ambaye ni Msimamizi wa masuala ya kisheria wa UNOC amesema mradi huu ulianza kujadiliwa takriban miaka 13 iliyopita, huku kukiwa na vikwazo vya hapa na pale, lakini hatimaye unaenda kukamilika ndani ya muda mchache ujao.

“Tunategemea mradi huu kuisha mwishoni mwa mwaka ujao kwa hatua hii ya kasi ya maendeleo inayoendelea sasa kwa pande zote (Uganda na Tanzania),” amesema.

Naye mjumbe wa bodi wa UNOC, Zulaika Kassajja amesema ni furaha isiyoelezeka kuona mradi huu unaenda kukamilika na kuweka historia.

“Tulianza kwa kufanya tathmini na baadae kuwalipa watu walioguswa na mradi huu na sasa tunashuhudia ujenzi unaendelea katika nchi zetu ili uanze kazi na hizi kufaidika,”

“Utekelezaji wa mradi huu kati ya Uganda na Tanzania ni kielelezo tosha cha ushirikiano uliopo kati ya Uganda na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo,”, amesema.

Kwa upande wa EACOP, Afisa wa Biashara wa mradi huu Bertrand Hertzog amesema ni furaha kuona watekelezaji wa mradi huu wanafuatilia maendeleo yake ili namna kazi zinavyoendelea katika maeneo mbalimbali ya ujenzi wake.

“Tunategemea mpaka mwakani mwishoni tuwe tumekamilisha ujenzi wa matenki na sehemu ya kufikia meli za kupakia mafuta na kukamilisha kila kitu ifikapo 2026,” amesema.

Mmoja wa wasimamizi wa eneo la mradi la Chongoleani, Remi Beziana amesema mradi wa EACOP umezingatia matakwa yote ya kimataifa,ikiwemo kuwajengea uwezo wazawa wakiwemo wanawake  kupitia mafunzo mbalimbali na kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya mradi katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama vile uboreshaji wa barabara na miradi ya maji safi na salama.

Lakini pia mradi kwa unazingatia uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kuweka vifaa maalum kwa kuzuia kelele za vitendea kazi, kutoa elimu ya uhifadhi mazingira kwa wananchi wanaozunguka mradi, kuweka vifaa maalum vya kuhifadhia aina mbalimbali za taka na kulinda viumbe vinavyoishi maeneo ya mradi ikiwemo wale wa baharini.

Mradi wa ujenzi wa bomba la EACOP una jumla ya urefu wa kilomita 1443, kati ya kilomita hizo, 1143 zipo nchini Tanzania na zilizobaki 296 zipo nchini Uganda.

Kwa upande wa Tanzania, mradi unapita katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Leave a Reply