Serikali ya Uganda imesema itaiondoa kesi dhidi ya mpinzani mkongwe Kizza Besigye katika mahakama ya kijeshi, na kumtaka asitishe mgomo wa kula gerezani.
Ahadi hiyo imetupiliwa mbali na mke wa Besigye ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la UNAIDS, Winnie Byanyima, akisema “inatia mashaka”.
Besigye, mshirika wa zamani wa Rais Yoweri Museveni ambaye aliyegeuka kuwa mpinzani wake wa muda mrefu, alianza mgomo wa kula tarehe 10 Februari kama njia ya kupinga kufungwa kwake.
Ikimtuhumu kwa uhaini kwa madai ya kutishia usalama wa taifa, serikali iliapa kumshtaki katika mahakama ya kijeshi, licha ya Mahakama ya Juu kutoa uamuzi kwamba hatua hiyo dhidi ya raia wa kawaida inakiuka katiba.
Sasa, hata hivyo, “serikali inaharakisha uhamishaji wa kesi ya Besigye kuiondoa katika mahakama ya kijeshi na kuipeleka kwenye mahakama ya kiraia”, msemaji wa baraza la mawaziri na waziri wa habari Chris Baryomunsi aliiambia AFP.
“Kama serikali, tunatekeleza uamuzi wa Mahakama ya Juu.”
Waziri huyo alisema katika ujumbe wa awali kwenye mtandao wa X kwamba alikuwa amemtembelea Besigye gerezani Jumapili “mbele ya madakatari wake wa kibinafsi” na “akamuomba aanze tena kula” kwa kusubiri uhamishaji wa kesi hiyo.