Maboresho yaliyofanywa na Mamlaka ya Bandari (TPA) katika bandari ya Mtwara yamevutia meli nyingi za kigeni katika usafirishaji wa korosho kwenda katika masoko ya kimataifa na kuufanya msimu wa 2024/2025 wa zao hilo la biashara kuwa wa mafanikio.
Mafanikio haya yanatokana na maboresho ya bandari hiyo yanayofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusaidia ukuaji wa biashara ya korosho zinazozalishwa katika Mikoa ya Kusini kwenye masoko ya kimataifa.
Mmoja wa wafanyabishara wa Korosho mkoani Mtwara wanaoitumia bandari hiyo kusafirisha mizigo yao, Omega Makanjiro amesema kuwa uwekezaji huu umewezesha meli tatu kuhudumiwa kwa wakati mmoja katika gati mpya na ya zamani, jambo lililochangia kwa kampuni nyingi za meli kupeleka meli zao katika Bandari ya Mtwara na wao kama wafanyabishara kusafirisha biashara zao kwa urahisi.
Ameipongeza TPA kwa juhudi zao za kuboresha huduma katika bandari hiyo na kuishauri iendelee kuitangaza kutokana na huduma zake zilizoboreshwa, ili kuvutia kampuni nyingine za meli zaidi.
Naye Herman Colman kutoka kampuni ya ETG, amesema kuwa msimu huu umekuwa mzuri zaidi kwao, kwani tangu kuanza kwa msimu huu, wameshasafirisha tani 40,000, ikilinganishwa na tani 26,000 walizosafirisha katika msimu uliopita.
“Hii inatokana na uboreshaji wa huduma na uwepo wa meli za kutosha katika kutoa huduma.
“Tunachukua na kusafirisha mizigo yetu kwa wakati na hii inapunguza gharama kwa mteja, ambaye ndio mtumiaji wa mwisho,” amesema.
Ameipongeza TPA kwa kuongeza mitambo na mashine za kisasa, jambo lililoongeza ufanisi na uwezo wa kuhudumia shehena nyingi kwa wakati.
Kutokana na maboresho mbalimbali yaliyofanywa na TPA katika bandari hiyo, msimu huu wa korosho umeleta mabadiliko makubwa kwa kuongeza idadi ya kampuni zinazotumia Bandari hiyo ya ukanda wa Kusini.
Katika msimu wa 2023/2024, kampuni tatu tu (PIL, MSC, na CMA CGM) zilikuwa zinasafirisha korosho katika bandari hiyo.
Lakini msimu huu wa 2024/2025, idadi ya kampuni za meli imeongezeka hadi saba (7). Kampuni hizo ni CMA CGM, MSC, PIL, ESL, ECSL, na COSCO.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, amethibitisha kuwa uzalishaji wa korosho umeongezeka mwaka huu, na hadi sasa, wameuza tani 238,000.
Aliongeza kuwa hakuna changamoto yoyote ya meli au makasha ya kubeba korosho kwa msimu huu, tofauti na misimu ya nyuma.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wanunuzi na wasafirishaji ni muhimu ili kuhakikisha msimu huu unakuwa endelevu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuinua hali za wakulima.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba 2024, TPA kupitia Bandari ya Mtwara imeshahudumia shehena ya korosho ghafi tani 133,000 kwa ajili ya masoko ya kimataifa, ongezeko kubwa la tani 72,921, ikilinganishwa na tani 60,079 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kwa mujibu wa TPA, hili ni ongezeko la asilimia 121. Taarifa ya TPA imeongeza zaidi kuwa meli 17 tayari zimefika na kuhudumiwa katika Bandari hiyona kati ya hizo, 14 zimepakia shehena ya makasha (Container Vessels), huku tatu zikibeba korosho zilizopakiliwa kwa magunia.
Taarifa hiyo zaidi imesema kuwa jumla ya makasha 3,366 tayari yamepakiliwa na kuondoka kutoka Bandari ya Mtwara, kati ya makasha 7,621 yaliyopo katika bandari hiyo kwa ajili ya kubeba zao hilo la biashara.
Serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 157.8 katika maboresho ya Bandari ya Mtwara na mafanikio haya ni sehemu ya matokeo ya uwekezaji huo.
Kabla ya uwekezaji huu, korosho zote kutoka Mikoa ya Kusini zililazimika kusafirishwa kwa malori hadi Dar es Salaam ili zisiweze kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa.