You are currently viewing Trump kuapishwa ndani ya jengo la bunge leo

Trump kuapishwa ndani ya jengo la bunge leo

RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kuapishwa leo Januari 20, 2025 kuwa rais wa 47 wa taifa hilo kubwa duniani ambapo uapisho huo utafanyika ndani ya jengo la Bunge la Capitol, kutokana na hali ya baridi kali katika Jiji la Washington DC.

Trump anarudi White House kwa mara ya pili baada ya kushindwa kwenye uchaguzi na Joe Biden ambapo aliongoza kwa muhula mmoja akiwa rais wa 45 kati ya mwaka 2017 hadi 2021.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 40 kwa rais mteule kuapishwa ndani ya jengo badala ya kwenye eneo la wazi tangu mwaka 1985 wakati Rais Ronald Reagan alipoapishwa ndani ya jengo akianza muhula wake wa pili.

Hafla ya uapisho itatanguliwa na maonesho ya muziki na hotuba ya ufunguzi kwenye jukwaa kuu lililopo kwenye majengo ya bunge la Marekani.

Kisha itafuatiwa na kuapishwa kwa Trump na makamu wa rais JD Vance pamoja na hotuba ya kuapishwa.

Kisha Trump ataingia Chumba cha Rais kutia saini hati muhimu za kuanza utawala wake mpya. Na baada ya chakula cha mchana ambacho rais atahudhuria, gwaride litaanza, kutoka majengo ya Bunge (Capitol) hadi Ikulu ya White.

Leave a Reply