You are currently viewing Trump akata rufaa dhidi ya mfanyakazi aliyemburuza mahakamani

Trump akata rufaa dhidi ya mfanyakazi aliyemburuza mahakamani

Rais Donald Trump amepeleka ombi la dharura katika Mahakama ya Juu ya Marekani ili iamue ikiwa ana mamlaka ya kumfukuza kazi mmoja wa viongozi waandamizi serikalini.

Hampton Dellinger, mtendaji Mkuu wa Ofisi ya mwanasheria maalumu, amemshtaki Trump baada ya kufutwa kazi kupitia barua pepe mwezi huu.

Trump pia amewafukuza wakaguzi wakuu kadhaa katika mashirika mbalimbali ya serikali pamoja na maelfu ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani.

Bw. Dellinger, aliyeteuliwa na rais wa zamani Joe Biden, amesema kufutwa kwake kunakiuka sheria inayowalinda viongozi wa mashirika huru dhidi ya kufutwa kazi na rais, isipokuwa katika kesi za uzembe wa kazi, matumizi mabaya ya madaraka, au kutoendana na majukumu yao.

Jaji wa shirikisho mjini Washington DC alitoa amri ya muda Jumatano inayomruhusu Dellinger kuendelea na kazi yake huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.

Juhudi za Trump kupunguza na kurekebisha mfumo wa utawala wa kiraia wa wafanyakazi wa serikali takriban milioni 2.3 ziliendelea mwishoni mwa wiki.

Wafanyakazi katika mashirika mbalimbali ya afya waliokuwa bado kwenye kipindi cha majaribio walipokea barua Jumamosi usiku wakifahamishwa kuwa watafutwa kazi, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyozungumza na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Trump tayari amefukuza wafanyakazi wasiopungua 9,500 katika wizara za Afya na huduma za binadamu, nishati, masuala ya wanajeshi wastaafu, mambo ya ndani, na Kilimo.

Aidha, wafanyakazi wengine wapatao 75,000 wamepokea ofa ya kuondoka kwa hiari yao kwa kupewa malipo maalum, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.

Mpango huu wa kupunguza gharama unapendekezwa na Idara ya Ufanisi wa Serikali (Department of Government Efficiency), au kwa kifupi Doge, kikosi kazi kinachoongozwa na Elon Musk.

Leave a Reply