You are currently viewing TRA yakusanya Sh bilioni 71.5 kwa miezi sita Kariakoo

TRA yakusanya Sh bilioni 71.5 kwa miezi sita Kariakoo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 71.5 sawa na asilimia 104 katika kipindi cha miezi sita cha mwaka mpya wa fedha 2024/25 kutoka eneo la kimkakati la mkoa Maalumu wa Kodi Kariakoo.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mcha Hassan Mcha amesema hayo jana Jumapili Dar es Salaam alipofungua bonanza lililoandaliwa na mamlaka hiyo likishirikisha wafanyabiashara wa Mkoa wa Kodi wa Kariakoo yakiwa ni maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya siku ya mlipa kodi.

Mcha amesema kuwa mkoa wa Kodi Kariakoo ni  eneo la kimkakati la serikali na TRA lenye wafanyabiashara zaidi ya 30,000.

“Mkoa wa Kodi Kariakoo ulianzishwa rasmi mwaka 2018, ukiwa ni mkoa wa kimkakati katika ukusanyaji kodi. Kwa kipindi cha miezi sita cha Julai 2024/25 TRA imepata mapato ya Sh. bilioni 71.5 sawa na asilimia 104 ya lengo,” alieleza Mcha.

Amesema mkoa huo wa kikod una ni lengo muhimu katika ukusanyaji mapato hapa nchini hususan kutengeneza wafanyabiashara mabilionea wapya.

“Ninawashukuru wafanyabiashara wote wa Kariakoo kwa niaba ya wafanyabiashara wote Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia. Mafanikio haya ni kwa sababu yao. Wanaotoa fedha ni wao na kazi yetu sisi TRA ni kukusanya,” alisema Mcha.

Alisema kulipa kodi ni uzalendo na uzalendo huo ni chachu ya ujenzi wa taifa ambapo mwananchi ana wajibu wa kulijenga taifa lake kwa kulipa kodi.

Awali, katika bonanza hilo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo aliwataka wafanyabiashara Kariakoo kuchangamkia fursa katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28 mwaka huu.

Amesema Rais Samia amekuwa kinara katika matumizi ya nishati safi, hivyo kuanzia Januari 26 Tanzania itaanza kupokea wageni wakiwemo marais kutoka nchi za Afrika ambao  watahudhuria mkutano huo.

“Ninawaomba wafanyabiashara kujiandaa kupokea wageni hawa, mkutano huo utahudhuriwa na marais kutoka nchi nyingi za Afrika ambao watapenda kufika Kariakoo au kutuma wawakilishi wao hivyo ni vyema  wafanyabiashara wa Kariakoo kujiandaa kimataifa,” alieleza.

Mwenyekiti wa Jumuiya Wafanyabiashara Kariakoo, Seveline Mushi, alisema wataendelea kushirikiana na TRA na serikali kwa kulipa kodi kwa wakati.

Leave a Reply