You are currently viewing TPA yafungua milango kwa  sekta binafsi kuchangamkia fursa bandarini

TPA yafungua milango kwa  sekta binafsi kuchangamkia fursa bandarini

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari  nchini (TPA) imeitaka sekta binafsi Tanzania kutumia fursa ya maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kufanya biashara na kuongeza mapato ya taifa kuinua uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Umoja wa Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Kaimu  Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus amesema maboresho yaliyofanywa yamekidhi vigezo, mahitaji na matarajio ya wafanyabishara na kuiweka bandari kwenye ushindaji wa kimataifa.

Gallus ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa alisema uwekezaji mkubwa  umefanywa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye miundombinu kama eneo la upakuaji na upakiaji  mizigo  kwa kutumia vifaa vya kisasa, ambapo kazi hiyo kwa sasa inafanyika ndani ya muda mfupi tofauti na hapo awali.

“Mashine za kupikia na kushusha mizigo yaani ‘Cranes’ zimerahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi mkubwa bandarini hapa. Ni nafasi ya pekee kwa sekta binafsi kuchangamkia,” Gallus alisema.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema TPA ina  mpango wa kujenga bandari kavu (ICDs) katika eneo la Shimo la Udongo Kurasini  jijini  hapa kwa ajili ya kuhifadhia mizigo inayoharibika kwa haraka (perishable goods) kama vile matunda katika vyumba maalum vyenye ubaridi.

 “Huko nyuma, mizigo ya bidhaa zinazowahi kuharibika ilikuwa inapitia katika bandari ya nchi jirani, lakini hivi sasa mizigo hiyo itakuwa inahifadhiwa katika bandari kavu ikisubiri  kusafirishwa kwenda nje ya nchi,” amesema.

“Kufuatia maboresho tuliyoyafanya, hivi sasa hakuna tena malalamiko ya kuchelewa kutolewa kwa mizigo inayowasili bandarini na badala yake, kutokana na kasi ya utendaji iliyopo, wateja ndio wanaochelewa kuja kuchukua mizigo yao,”

Alisema TPA ina maeneo makubwa ya kuhifadhi mizigo na kutoawito kwa wafanyabishara kuchukua mizigo yao kwa wakati bandarini kwani bandari siyo  sehemu ya kuhifadhi mizigo kwani mizigo yote ya wateja inatakiwa itoke ili kutoa nafasi kwa mizigo mingine.

 “Kasi ya ushushaji wa shehena itaboreka zaidi wateja watakapochukua mizigo yao kwa wakati,” amesema Gallus alisema na kuongeza kuwa TPA imejipanga na itaendelea kuwa lango imara la Uchumi.

 Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, moja ya kampuni  iliyowekeza katika bandari hiyo ya Dar es Salaam, Elitunu Mallamia amesema kinachotokea sasa hivi katika bandari ya Dar es Salaam  ni mizigo kusubiri wateja kuondolewa na siyo uchelewashaji tena kutokana na kasi ya utendaji iliyopo.

  “Tumeweza kuhudumia shehena asilimia 25 zaidi kwenye miezi hii ambayo tumefanya kazi kuanzia mwezi Mei 2024  mpaka sasa Januari 2025),”Bw Mellamia alisema  na kuongeza kuwa  kwa mwezi Desemba pekee   magari 25,251 yalishushwa kwenye  meli 16 na kuvunja rekodi.

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa wafanyabiashara, Hamis Livembe aliipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuleta mageuzi makubwa kwenye bandari zote hapa nchini. 

 “Miaka miwili iliyopita, tulikuwa na kilio cha ucheleweshwaji wa mizigo kutoka bandarini na wakati mwingine biashara zilichelewa kuwafikia wateja kwa wakati,” alisema nas kuongeza kuwa  maboresho yaliyofanyika yameleta suluhisho la kudumu. 

Leave a Reply