Mbunge wa Mafinga na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi (CCM) ametembelea TFS-Shamba la Miti Sao Hill na kuwataka wahifadhi kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaolizunguka ili kuendeleza uhusiano mzuri iliopo baina ya Shamba na wananchi.
Pia ameipongeza TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill kwani imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwa wakazi wanaolizunguka shamba hasa ikizingatiwa kwani limechangia uendelezaji wa miradi mingi ya maendeleo hususani katika Wilaya ya Mufindi na Taifa kwa ujumla.

Chumi ametoa pongezi hizo leo tarehe 3 Januari alipotembelea shamba hilo ili kuona namna shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa misitu zinazofanywa.
Aidha, amesema Shamba la Miti Sao Hill limekuwa msingi mkubwa wa uzalishaji wa malighafi za viwanda hali iliyochangia kukua na kuongezeka kwa uwekezaji wa viwanda vya mazao ya misitu katika Wilaya ya Mufindi.

Pia amewataka wahifadhi kuongeza jitihada za ulinzi wa rasilimali misitu dhidi ya majanga ya moto yanayoweza kujitokeza na ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na kuharibu rasilimali hiyo.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi wa ngazi zote Wilayani Mufindi kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinafanyika kwa ufasaha na kuhakikisha elimu ya uhifadhi inawafikia wananchi wote.