You are currently viewing  Tanzania yaingia tatu bora nchi za Afrika kwenye mashindano

 Tanzania yaingia tatu bora nchi za Afrika kwenye mashindano

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika ambazo zimefanikiwa kuingiza timu zake kwenye michuano ya kimataifa zaidi ya saba kwa wakati mmoja.

Prof. Kabudi amesema hayo Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya sekta ya michezo katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ameeleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwezeshwaji wa shilingi bilioni 161 ambazo zimechagiza uendelezaji wa sekta hiyo.

Prof. Kabudi ametaja timu hizo za Taifa za Tanzania ambazo zimefuzu na kushiriki michuano mbalimbali ya Kimataifa kuwa ni Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu (Taifa Stars), Twiga stars kwenda michuano ya mpira wa Wanawake (WAFCON), Ngorongoro Heroes U20, Serengeti boys, Timu ya Taifa ya mpira wa ufukweni, Taifa Stars kufuzu CHAN 2024 na Taifa Stars kufuzu kushiriki michuano ya kombe la dunia nchini Morocco.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi 3 barani Afrika ambazo zimefanikiwa kufuzu kuwania michuano ya kimataifa ikiwa pamoja na Senegal na Morocco, Tanzania inang’ara” amesisitza Prof. Kabudi.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amesema kufanyika  kwa michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027 ni mafanikio mengine ya Serikali ya awamu ya sita akibainisha kuwa yatakapofanyika nchini Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, yatachagiza ajira kwa vijana na utalii katika sekta ya Michezo.

Leave a Reply