Imeelezwa kuwa, mradi wa kufua umeme unaotokana na maji wa Rusumo, umeanza kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa megawati 26.6 kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha gridi za Taifa za umeme.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda, amesema hayo wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo uliopo Wilaya ya Ngara katika Mkoa wa Kagera.
Amesema mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya RPCL inayomilikiwa na nchi zote tatu ni kielelezo cha azma ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kijamii.
Aidha, Ng’enda amewataka watekelezaji wa mradi kuendelea kufanya kazi kwa tija na kuhakikisha matumizi ya fedha yanaendana na maendeleo ya mradi, pia umuhimu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya kijamii (CSR).
Kamati imeeleza kuridhishwa kwake na mafanikio ya mradi huo na hatua iliyofikiwa katika uendeshaji wa pamoja, jambo litakalosaidia kuimarisha pia uhusiano mzuri baina ya nchi hizo tatu.
Vilevile Kamati imepongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania, Burundi na Rwanda katika kuchochea maendeleo ya uchumi na kudumisha amani, undugu na urafiki wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Dk. Khatibu Kazungu, amewashukuru Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge kwa ufuatiliaji na ukaguzi wa mradi huo ambao una maslahi mapana kwa Taifa zima.
Aidha, ameahidi kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kuyafanyia kazi maelekezo yanayotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo ili kuzidi kuongeza ufanisi wa Sekta ya Nishati.