You are currently viewing RITA yamaliza mgogoro wa  msikiti wa Ijumaa Mwanza

RITA yamaliza mgogoro wa  msikiti wa Ijumaa Mwanza

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

 Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhani nchini (RITA), umeitaka Bodi mpya ya Wadhamini wa Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza, kujiepusha na ubadhirifu wa mali za msikiti sambamba na kuimarisha mshikamano wa waumini, pamoja na kutolipiza visasi kwa bodi ya wadhamini ya msikiti huo iliyovunjwa awali.

 Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa bodi mpya ya msikiti wa Ijumaa Jijini hapa,   Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa (RITA), Frank Kanyusi alisema uteuzi wa bodi hiyo mpya umejili baada ya kuwepo kwa mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30, baada ya kufanyika usajili wa mabadiliko ya katiba mnamo mwaka 1990.

“Sababu zinazotajwa kusabishwa migogoro hiyo, ni kutotambulika mabadiliko ya Katiba ya mwaka 1993 yaliyowasilishwa kwa Msajili Mkuu mwaka 1997, kutoelewana wajumbe wa bodi ya wadhamini iliyokuwepo, matumizi mabaya ya mali, fedha na kukosekana kwa uwazi katika Taasisi,” alisema Kanyusi.

Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa (RITA), Frank Kanyusi, akiwa kwemye picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi mpya ya Udhamini ya msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza na wajumbe wa Kamati ya Mpito ya msikiti huo iliyomaliza muda wake wa uongozi.

Alisema Tarehe 2 mwezi  Februari mwaka huu, RITA iliunda kamati ya uchunguzi ambayo ilifanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja   na kukabidhi ripoti iliyoonyesha kuna ubadhirifu wa fedha takribani shilingi bilioni moja ya kitanzania.

“Baada ya tuhuma  zilizokuwa zikiikabili bodi iliyopita niliunda kamati ya  uchunguzi iliyowasilisha  taarifa kwa mamlaka za uchunguzi (TAKUKURU)  ambapo mpaka sasa kazi imeshaanza  kufanyika, na baadhi ya wajumbe wa bodi iliyopita wameshahojiwa, na hivi punde TAKUKURU itakamilisha  kazi yake na  wataka bainika katika ubadhirifu huo taratibu za kisheria zitafuatwa ili kila mmoja apate  stahiki kwa mujibu wa sheria.” alieleza Kanyusi.

Kanyusi alitoa rai kwa  wajumbe wa bodi mpya   ya udhamini    kuhakikisha   wanatekeleza majukumu yao  kama sheria inavyotaka,  alisisitiza kuwa wao sio wamiliki  wa  mali  bali ni wasimamizi  wa mali kwa niaba ya  wanachama  hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kabidhi Wasii Mkuu huyo amewashukuru na kuwapongeza waumini wa msikiti huo kwa ustaarabu na utulivu mkubwa waliouonyesha kwa kipindi chote cha kamati ya uongozi wa mpito.

 Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti Bodi Mpya ya Wadhamini ya Msikiti wa Ijumaa, Sherally Hussein mbali ya kuipongeza RITA kwa usimamizi mzuri alisema  wakati umefika wa kuunganisha nguvu kwa waislamu wote wa msikiti huo ili   kusimamia malengo yaliyo kusudiwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Kabidhi Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa (RITA) Frank Kanyusi, akizungumza na waumimi wa msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza.

“kwa sasa tuna imani kwani ile mivutano  ilitugawa kwa makundi tofauti tofauti, ni wakati sahihi sasa makundi yote kuungana ili  taasisi yetu iweze kutoe mchango stahiki kwa waumini  wote  na taifa kwa ujumla wake,” alisema Hussein.

Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu nchini (RITA) imeahidi kuendelea kutoa  ushirikiano kwa bodi mpya ya wadhamini katika uongozi ili iweze kutimiza majukumu yake kikamilifu kwa maslahi mapana ya waumini  ya jumuiya ya kiislam mkoa wa Mwanza.

Leave a Reply