Netumbo Nandi-Ndaitwah ameapishwa kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba mwaka jana ambao unarefusha utawala chama cha SWAPO kilichopigania uhuru wa taifa hilo.
Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72 anakuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Namibia na miongoni mwa wanawake wachache waliowahi kushika wadhifa wa urais kwenye mataifa barani Afrika.
Halfa ya kuapishwa kwake imefanyika ikulu ya nchi hiyo mjini Windhoek na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi kadhaa wa Afrika akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye hadi leo alikuwa ndiye rais pekee mwanamke barani humo.
Nandi-Ndaitwah ambaye hapo kabla alishikilia nafasi ya makamu wa rais, ni kada wa muda mrefu wa chama cha ukombozi wa watu wa Namibia cha SWAPO kilichoiwezesha nchi hiyo kupata huru kutoka Afrika Kusini mwaka 1990.