You are currently viewing Rais Samia kutua Marekani kujadili changamoto za chakula

Rais Samia kutua Marekani kujadili changamoto za chakula

Rais Samia Suluhu Hasan anatarajia kuondoka nchini leo tarehe 29 Oktoba, 2024 kuelekea Des Moines, lowa, nchini Marekani kuhudhuria Mjadala wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug ulioandaliwa na Taasisi ya World Food Prize Foundation ya nchini humo.

Mjadala wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug hufanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na viongozi, wataalamu, watu mashuhuri, watunga sera, hususan za kilimo, lishe na usimamizi wa rasilimali.

Shabaha ya majadiliano hayo ni kutafuta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa chakula duniani, ambayo inachochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Rais Dk. Samia ni miongoni mwa Marais wanne kutoka Afrika, waliopewa heshima ya kushiriki na kuchangia kwenye mjadala huo wenye kaulimbiu isemayo: Mbegu za Fursa: Kuunganisha Vizazi na Kustawisha Diplomasia (Seeds of Opportunity: Bridging Generations and Cultivating Diplomacy.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Sharifa Nyanga imesema viongozi wengine watakaoshiriki ni kutoka nchi za Sierra Leone, Madagascar na Nigeria.

Mbali na mjadala huo, Rais Dk. Samia pia atashiriki hafla ya utoaji tuzo ya World Food Prize kwa mwaka 2024 kwa watu wenye mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, ikiwa ni mwendelezo wa kumuenzi Hayati Dk. Norman E. Borlaug aliychamasisha usalama wa chakula duniani kwa watu wote.

Sambamba na kushiriki kwenye majadiliano hayo, Rais Dkt. Samia atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi kutoka Serikali na sekta binafsi ya Marekani, hususan waliopo kwenye sekta ya kilimo kwa lengo la kujadili uwekezaji katika sekta hiyo na kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Leave a Reply