Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuendeleza kasi ya uhamasishaji uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura na kuhakikisha vijana wengi wanajiandikisha litakapoanza kwa upande wa Unguja hivi karibuni.
Ametoa wito kwa vijana kutobaki nyuma siku ya kupiga kura ili CCM ipate ushindi wa kihistoria na kuendelea kushika dola.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo jana Jumatatu alipozungumza na wanachama wa chama hicho katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la Bweni la Vijana wa Kiume wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni lazima chama nacho kiache alama ya uongozi itakayokumbukwa kwa muda mrefu kwa kufanya mambo makubwa ya maendeleo na miradi ya chama katika ngazi zote.
Aidha, Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa alama iliyoachwa na Serikali katika sekta zote za Maendeleo ni lazima pia iachwe ndani ya CCM.
Kwa upande mwingine Dkt. Mwinyi amesema CCM kitaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya hiyo kwa hali na mali ili dhamira ya kuwajenga vijana kuwa wazalendo na kuwapatia mafunzo mbalimbali ifanikiwe.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Ali Kawaida amesema Kauli ya Mitano Tenani kwa ajili ya viongozi wawili tu ndani ya CCM ambao ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Mwenyekiti CCM Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi.