SIKU moja baada ya Tundu Lissu kushinda nafasi ya Uenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakili huyo amedaiwa kushindwa kulipa gharama za Ukumbi wa Mlimani City walipokuwa wakifanya mikutano yao ya uchaguzi sambamba na Baraza Kuu la chama hicho.
Mbali na gharama hizo za ukumbi, pia baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wamedaiwa kuhaha kutafuta fedha kukomboa mali zao kwenye hoteli waliozokuwa wamefikia.
Imeelezwa kuwa mara baada ya Lissu kutangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wajumbe waligawanyika na wengine walivyokwenda kwa ajili ya kupata malipo yao walielezwa kuwa chama hakina fedha.
“Hapa nilipo sijui nitafanyaje, baada ya matokeo tuliambiwa fedha tulizolipwa za kujikimu kwa siku mbili ndio zimeishia hapo, tukaambiwa tujitegemee, ninavyoongea na wewe mabegi yangu yameshikiliwa natakiwa kulipa fedha, bado natakiwa kujilipia nauli kurudi nilikotoka,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.