You are currently viewing Pemba yaanza kupokea meli za mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji

Pemba yaanza kupokea meli za mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Meli ya kwanza ya makontena imetia nanga katika Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba na kupokewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

Licha ya kuwapo bandari kubwa mbili katika kisiwa cha Pemba, hapo awali hazikuwa na uwezo wa kupokea meli za mizigo isipokuwa tu za abiria.

Uwekezaji uliowezesha bandari hiyo kuanza kutumika, utarahisisha kusafirishaji mizigo moja kwa moja kwenda nje na kuinmgia, na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali na wafanyabiashara.

Kwa maana hiyo, bidhaa kama vile karafuu, mwani, samaki na rasilimali nyingine zitasafirishwa kwenda nje bila kulazimika kupitia Malindi, Unguja.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Jumatatu Septemba 30, 2024, Rais Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema hatua hiyo ni muhimu inayotoa fursa zaidi kwa wafanyabiasha na wananchi wa Unguja na Pemba kunufaika na jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za bandari.

Amesema Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi katika kuendesha huduma za bandari kwa kutambua bandari ni lango kuu la uchumi kwa nchi.

“Malengo ya kuweka mkazo katika ufunguzi wa bandari hii ya Mkoani pamoja na bandari zingine zote za Unguja na Pemba, ni kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, ili kukuza uchumi na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine kama vile utalii, biashara, ujenzi, uchukuzi na uwekezaji,” amesema.  

Amesema katika kutekeleza malengo ya nchi, Serikali inakusudia kuimarisha huduma za bandari kwa kutumia vifaa vya kisasa vyenye ufanisi na uwezo mkubwa, ili kuongeza idadi ya makontena kutoka 82,312 mwaka 2018 hadi kufikia 105,000 ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Rais  Mwinyi, uwekezaji huo pia unafanywa kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya kutoa nafasi kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuendesha shughuli za bandari. 

Amesema Kampuni ya Fumba Port Ltd, imekabidhiwa rasmi kazi ya utoaji wa huduma ya kupakia na kushusha makontena katika Bandari ya Mkoani ambapo takriban ya makontena 45.

Katika hatua za kukarabati bandari hii, Serikali kupitia Shirika la Bandari Zanzibar imetumia Sh6.4 bilioni na kazi zilizofanyika ni pamoja na kujenga sehemu ya kuhifadhi makontena yenye ukubwa wa mita za mraba 4,200 yenye uzio wenye mfumo wa usalama wa umeme na inayoweza kuhifadhi makontena 580 kwa kubebesha matatu kwenda juu.

Kazi nyingine ni kuweka njia ya kupitia abiria yenye urefu wa mita 300 na upana wa mita 2.5, ambayo ina paa juu ili kuzuia mvua na jua.

Pia, Serikali imetumia Sh4.874 bilioni kununua vifaa vya kushushia na kupandisha makontena.

Dk Mwinyi amesema mwekezaji huyo atafanya mabadiliko katika bandari hiyo kwa kujenga jengo la abiria, kutanua gati ya mizigo, kujenga maghala ya kuhifadhia mizigo, kuandaa mpango kabambe wa utanuzi wa bandari hiyo, ambayo itajumuisha maeneo ya forodha na viwanda vidogo vya kuchakata bidhaa na kuongeza thamani.

Kitu kingine atakachokifanya, atatenga eneo la ghala la vitu vinavyohitaji baridi kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa za bahari na kilimo, pamoja na kununua vifaa vitakavyowezesha Bandari ya Mkoani kuhudumia hadi makasha 30,000 kwa mwaka. 

Ametumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kusimamia kwa ubora ili iendelee kuleta tija kwa wananchi na Serikali.

Awali, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum amesema uzinduzi wa bandari hiyo utafungua fursa nyingi katika mkoa huo katika usafirishaji wa biashara.

Leave a Reply