You are currently viewing NMB yakabidhi vifaa vya michezo vya Mil. 19/- kwa timu za JWTZ

NMB yakabidhi vifaa vya michezo vya Mil. 19/- kwa timu za JWTZ

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeishukuru Benki ya NMB kwa namna inavyojitoa kuunga mkono Sekta ya Michezo ndani ya jeshi hilo, kwa kufadhili na kuwezesha ushiriki wa Timu za Majeshi katika michuano mbalimbali, pamoja na kudhamini uendeshaji wa mashindano yake.

Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Utimamu wa Mwili, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa JWTZ Makao Makuu, Kanali David Luoga, wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Mil. 19 vilivyotolewa na NMB kwa ajili ya timu za vijana walio chini ya miaka 20 ya Mashujaa na Mashujaa Queens za JWTZ

Akimwakilisha Mkuu wa Tawi la Oparesheni na Mafunzo Makao Makuu ya JWTZ, Meja Jenerali Ibrahim Mhona, Kanali Luoga alisema NMB imekuwa mdau kinara wa jeshi katika hatua mbalimbali za uendeshaji wa timu, ushiriki wa timu katika Mashindano ya Majeshi na udhamini kila wanapokuwa na uhitaji.

“Tunashukuru sana kwa sapoti hii inayotolewa na NMB kwa JWTZ na timu zake, mara nyingi wamefanya hivi katika ushiriki wa JWTZ michezoni na uendeshaji wa mashindano yake kwa ujumla na leo tuko hapa kudumisha michezo, ambayo sisi jeshini tunaifanya kupitia kaulimbiu ya; Michezo ni Furaha na Umoja.

“JWTZ tunaamini kuwa tukifanya michezo kwa kwa furaha na umoja, tutajenga nchi yetu kiuchumi, na katika hili, NMB mmekuwa wadau na wawezeshaji wetu wakubwa kutuwezesha kimichezo,” alisema Kanali Luoga mbele ya Mkuu wa Kikosi cha Usafirishaji na Mwenyekiti wa Mashujaa FC, Benjamin Kisinda.

Kanali Luoga alifafanua kuwa NMB wamekuwa wakidhamini wanapoendesha mashindano, yakiwemo CDF Trophy kwa mchezo wa gofu, Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) na CDF Cup, na kuwa wanajivunia sana mashirikiano yao na NMB, ambayo imekuwa kimbilio lao mara kwa mara tunapokuwa na ushiriki ama uhitaji.

“Tunashukuru kwa vifaa hivi tunavyopokea leo kwa ajili ya timu za Mashujaa FC Under 20 na Mashujaa Queens, ambavyo vitatumika katika maandalizi na michezo mbalimbali inyohusisha timu hizo. Msaada huu ni mkubwa mno, vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Mil. 19 sio jambo dogo, ni kubwa sana,” alisisitiza Kanali Luoga.

Akiahidi ushirikiano endelevu, Kanali Luoga akaiomba NMB kutowachoka na kuwataka kujiandaa kuwa sehemu ya CDF Cup 2025, inayotarajiwa kuanza Juni mwaka huu: “Tunatarajia sapoti yenu pia tunapojiandaa na CDF Cup 2025,” alisema mbele ya Luteni Kanali Penina Anthony Igwe, Afisa Mnadhimu wa Kurugenzi ya Michezo JWTZ.

Awali, Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi wa NMB, Ally Ngingite, aliipongeza JWT kwa kuwa na timu bora na imara zikiwa na muendelezo mzuri na hivyo kumpongeza Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda kwa juhudi zake za kukuza na kuimarisha michezo nchini.

“Kwa sasa michezo ni ajira yenye kuleta kipato kikubwa sana kwa washiriki, hivyo JWTZ kuwekeza katika sekta hiyo ni jambo la kizalendo. Na sisi kama wadau wenu katika kuunga mkono juhudi hizo, leo tunakabidhi msaada huu wa vifaa vya michezo, huku tukiahidi kudumisha uhusiano mwema baina ya taasisi hizi.

“Tuko hapa kukabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh. Mil. 19, vikiwemo jezi za kuchezea seti nne, ‘track suit’ 50, sare za kusafiria 40, nguo rasmi za timu 50, vizibao vya mazoezi ‘bips’ sanamu za mazoezi na glovu za magolikipa seti nane,” alisema Ngingite katika hafla hiyo.

Aliishukuru JWTZ kwa ushinrikiano endelevu uliopo baina ya NMB na jeshi hilo na kwamba udhamini wa miaka saba wa Mashindano ya Gofu ya CDF Trophy yanayofanyika Klabu ya Gofu Lugalo ni kielezo sio tu cha ukaribu wao, bali pia dhamira ya benki yake kukuza na kuimarisha Sekta ya Michezo Jeshini.

Leave a Reply