You are currently viewing Mradi JNHPP wafikia asilimia 99.55, megawati 1,175 zaingizwa gridi ya Taifa

Mradi JNHPP wafikia asilimia 99.55, megawati 1,175 zaingizwa gridi ya Taifa

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema utekelezaji wa Mradi wa Kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kwa ujumla umefikia asilimia 99.55 huku shughuli za uzalishaji wa umeme zikiwa zimeanza na wastani wa megawati 1175 zinazozalishwa kutoka mashine tano za mradi huo zikiwa zimeingizwa kwenye grid ya Taifa.

Hayo yamebainishwa jana Alhamisi na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga wakati uongozi wa shirika hilo ulipotembelea kujionea kasi ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kusisitiza wasimamizi kuhakikisha usimikaji wa mashine nne zilizobakia unafanyika ipasavyo ili umeme utakapozalishwa uingizwe kwenye Gridi ya Taifa kwa mafanikio  yatakayoleta tija inayotarajiwa kwa watumiaji wa umeme.

Alisema kwa sasa jumla ya mashine tano zimekamilika kwa asilimia 100 yaani mashine namba 9, 8, 7, 6 na 5 na tayari zimeanza uzalishaji wa umeme.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa usimikaji wa mashine namba 4 umefikia asilimia 100 ambapo kwa sasa mashine hiyo ipo kwenye majaribio huku mashine namba 3 ikiwa kwenye asilimia zaidi ya 87 za usimikwaji, asilimia ambazo zinadhihirisha kuwa kiwango cha utendaji kazi ni kizuri.

Aliwahimiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanaendeleza bidii  kusimamia maeneo ambayo bado hayajakamilika kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vilivyoainishwa wakati wa usanifu wa mradi huo.

“Niwaombe msimamie vizuri kuhakikisha ufanyaji kazi wa mashine unakuwa ni mzuri ili umeme unaoendelea kuzalishwa unapoungwa kwenye Gridi ya Taifa usilete changamoto yoyote ” alisisitiza Mha. Gissima.

Katika hatua nyingine, Mha. Gissima aliishukuru Serikali pamoja na wizara ya nishati na viongozi wake wote kwa namna ambavyo mara zote imeunga mkono kwa kutoa fedha na ushirikiano katika kusimamia utekelezaji wa mradi mpaka kufikia hatua iliyopo sasa pamoja na miradi mingine mingi inayoendelea nchini.

“Ninawaahidi watanzania wenzangu kuwa,  sisi kama  viongozi wa TANESCO tutahakikisha tunasimamia mradi huu kwa dhati na umadhubuti mkubwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta tija ya kiuchumi na kijamii katika taifa letu la Tanzania,” alihitimisha Mha. Gissima.

Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere tayari umeanza kuleta matumaini makubwa ya kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini ikiwa ni kati ya juhudi kubwa za Serikali.

Leave a Reply