You are currently viewing Moto wasababisha ndege 1,350 kushindwa kutua uwanja wa Heathrow

Moto wasababisha ndege 1,350 kushindwa kutua uwanja wa Heathrow

Uwanja wa ndege wa Heathrow uliopo katika jiji la London nchini Uingereza umefungwa kabisa Ijumaa kufuatia umeme kukatika kwa sababu ya moto uliozuka katika kituo kidogo cha umeme magharibi mwa London.

Kwa mujibu wa tovuti inayofuatilia safari za ndege mtandaoni Flightradar24, ndege kiasi 1,350 zilikuwa zimepangwa kutua katika uwanja wa Heathrow jijini London, Uingereza, au kupaa kutoka kwa maeneo matano ya kuondokea ndege leo Ijumaa. 

Abiria 230,000 kwa siku na milioni 83 kwa mwaka hutumia uwanja wa Heathrow, na hivyo kuufanya kuwa miongoni mwa viwanja vyenye shughuli nyingi duniani.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zimerekodiwa katika vituo vya abiria katika uwanja wa Heathrow, zimeonyesha maduka yaliyoharibiwa na njia zisizo na watu, zikiwa na taa zinazowashwa kunapotokea matukio ya dharura.

Kufungwa kwa uwanja huo kumewaacha abiria wengi waliokwama wakihangaika kutafuta na kufanya mipango mingine ya kuendelea na safari zao. 

Shirika la ndege la Uingereza British Airways limesema kufungwa kwa uwanja wa Heathrow kutakuwa na athari kubwa kwa shughuli zake pamoja na abiria wake. 

Waziri wa nishati wa Uingereza Ed Milliband amesema hakuna dalili zozote zinazoashiria kwamba kumefanyika hujuma yoyote. 

“Hakuna pendekezo lolote kwamba kuna mchezo mchafu. Hatujui sababu ya moto huu. Ni dhahiri ni tukio ambalo halijawahi kutokea. Lakini nadhani unachostahili kusema ni kwamba tutataka kuelewa sababu za tukio hili na ni masomo gani, ikiwa yapo, linaweza kutufundisha.”

“Kama ninavyosema, gridi ya taifa haijawahi kushuhudia tukio kama hili. Hivyo ni tukio la nadra sana ambali halikutarajiwa. Lakini ni wazi, huu ni usumbufu mkubwa kwa watu huko Heathrow. Na ila shaka kwa tukio kama hii, tutataka kujifunza masomo yanayofaa.” Aliongeza kusema Miliband.

Polisi wa Uingereza pia wamesema mpaka sasa hakuna ushahidi wowote unaoashiria kuna njama iliyofanyika kusababisha moto uliopelekea uwanja wandege wa Heathrow kufungwa, lakini ikaongeza kuwa kitengo chake cha kupambana na ugaidi kinaongoza uchunguzi ikizingatiwa ukubwa wa tukio lenyewe.

Katika taarifa yake polisi ya mjini London imesema kwa kuzingatia eneo la kituo cha umeme na athari za tukio la moto kwa miundombinu ya kitaifa, kamandi yake inayoshughulikia masuala ya ugaidi inaendelea na uchunguzi. 

Taarifa hiyo aidha imesema kitengo hicho kina raslimali za kutosha na uwezo kuendeleza uchunguzi huo kwa kasi na kwamba polisi wanashirikiana na idara ya zima moto ya London kutafuta chanzo cha moto huo.

Wachambuzi wanasema kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Heathrow kutasababisha athari kubwa katika usafiri wa anga ulimwenguni kote na uchumi wa Uingereza. John Strickland mtaalamu huru wa usafiri wa anga ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba safari za masafa marefu zimeathiriwa zaidi, huku ndege nyingi zikielekezwa zirejee katika viwanja vya nchi zilikotokea au sehemu nyingine za Ulaya mbali kabisa na uwanja wa mwisho wa safari ulionuiwa.

“Heathrow ndio uwanja mkubwa kabisa Uingereza na Ulaya. Ni miongoni mwa viwanja vikubwa vitano duniani. Huendesha shughuli zake kikamilifu katika masaa ya kawaida ya kazi, kwa hiyo kuufunga kwa saa 24 kunasababisha athari kubwa kwa usafiri wa anga na uchumi wa Uingereza.

Kiasi ndege 120 zilikuwa angani kuelekea Heathrow wakati tangazo la kufungwa uwanja huo lilipotolewa. Mamlaka za uwanja wa ndege wamesema wanatarajia usumbufu mkubwa na safari kutatizwa katika siku zijazo. Kiwanja cha pili kwa ukubwa cha Uingereza, Gatwick, kimesema kitapokea baadhi ya ndege kutoka Heathrow. Ndege nyingine zimeelekezwa katika viwanja vingine Ulaya ukiwemo Shannon kusini magharibi mwa Ireland, Frankfurt Ujerumani na Paris Charles de Gaulle.

Leave a Reply