Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Ijinga kilichopo kwenye kisiwani katika kata ya Kahangara Wilayani Magu mkoani Mwanza kuwa watafikishiwa umeme hivi karibuni baada ya Serikali kutenga kiasi cha Sh milioni 600 zitakazotumika kupeleka umeme wa jua (solar).
Amesema Kijiji hicho ambacho ndicho pekee ambacho hakijafikiwa na umeme, tayari Mkandarasi yupo eneo la mradi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo.
Dk. Biteko amebainisha hayo leo Jumatatu tarehe 23 Desemba 2024, Wilayani Magu wakati akihutubia wananchi katika Mkutano Mkuu Maalum ambapo taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa mwaka 2020 hadi 2024 iliwasilishwa.
“Mnavijiji 82, vijiji 81 vyote vina umeme kimebaki kijiji kimoja kipo kwenye kisiwa na tuliona itachukua muda kuwapelekea umeme kwa kulaza nyaya kwenye maji tukaona watu wa Ijinga ni Watanzania wanastahili kupata umeme tumetenga milioni 619 ili nao wapate umeme,” alisema
Biteko amesema Mkandarasi yupo eneo la mradi Kampuni ya Master Volt Ltd yupo kwa ajili ya kupeleka umeme Jua (Solar).
Ameongeza kuwa maendeleo katika Jimbo la Magu hayakuja kwa bahati mbaya isipokuwa kwa mipango na hivyo anawapongeza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Magu kwa tamko la pongezi kwa Rais Samia kwa kuwapa fedha kiasi cha shilingi 143.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha umeme katika vijiji 81 kati ya vijiji 82 jimboni humo.
“Kazi kubwa imefanyika, umeme sasa 99%, tumebakiza kijiji kimoja tu cha Ijinga kwani vijiji 81 tayari vyote vina umeme,” amesema.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kuibeba ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo alisema inakwenda kuokoa mazingira na afya zao.
“Naipongeza REA kwa kuibeba ajenda hii ya Mhe. Rais kwa kuandaa programu mbalimbali ikiwemo ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya 50%,” alisema Kiswaga.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini, Msimamizi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Awesa Rashid amesema REA inatekeleza miradi mbalimbali mkoani humo na kwamba baada ya kukamilisha kusambaza umeme vijijini na sasa ni zamu ya vitongoji.
“Tunatekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 15 kwa kila Jimbo ikiwemo Jimbo la Magu ambapo kwa sasa mradi huu unaendelea,” amefafanua Mhandisi Awesa.
Ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya shilingi 27,000 tu ili kujiletea maendeleo.