OPARESHENI maalumu iliyofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama imefanikisha kukamatwa magunia ya kufungia tumbaku maarufu kama majafafa yenye thamani ya zaidi ya sh bil 1.4.
Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Ji Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) amethibitisha kukamatwa marobota ya mali hizo na watuhumiwa 15 waliohusika na wizi huo wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Waziri Bashe ametaja baadhi ya watu waliohusika katika wizi huo wa mali za wakulima kuwa ni makampuni yanayonunua zao la tumbaku, taasisi za fedha, viongozi wa vyama vya Ushirika na viongozi wa kuchaguliwa na wananchi.
Amemwagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kuchukua hatua mara moja kwa kuwasimamisha kazi Viongozi wote wa vyama vya msingi (Amcos) na vyama vikuu vya ushirika (Union) waliohusika katika wizi huo wa mali za wakulima.
Amesisistiza kuwa kwa miaka 2 Wizara yake imekuwa ikifanya jitihada za kubaini mianya ya wizi wa mali za wakulima, juhudi hizo sasa zimezaa matunda baada ya kunaswa wezi na marobota ya magunia ambayo ni mali ya wakulima.
‘Majafafa ni mali ya wakulima, mnunuzi yeyote anaponunua tumbaku anapaswa kurudisha magunia hayo kwa mkulima ili ayatumie kufungia tumbaku yake msimu unaofuata na sio kumuuzia tena mara ya pili, huu ni wizi,’, ameeleza.
Waziri Bashe ameonya kuwa ni marufuku kwa kampuni yoyote, mabenki au viongozi wa ushirika kuwauzia majafafa kwa kuwa tayari waliyanunua msimu uliopita na wanaweza kuyatumia kwa miaka 2 au 3 kwa kuwa ni mali yao.
Amebainisha kuwa katika oparesheni hiyo iliyofanyika katika Mikoa ya Tabora na Shinyanga wamekamata malori yaliyokuwa yanasafirisha marobota ya magunia hayo, wahusika waliokuwa wakiyasafirisha na wamiliki wa magodauni.
‘Tutafanya uchunguzi wa kina kwa makampuni ya tumbaku, viongozi wa vyama vya ushirika, taasisi za fedha na wafanyabiashara wote, yeyote atakayebainika kufanya uhujumu huu atakiona cha moto na maghala yote yakamatwe’, ameeleza.
Amempongeza Mkuu wa Mkoa huo na timu yake ya vyombo vya dora iliyofanya oparesheni hiyo.