You are currently viewing Majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo SGR yakamilika

Majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo SGR yakamilika

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema kuwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo, yaliyowasili nchini Desemba 2024, yamekamilika.

Majaribio ya mabehewa hayo yaliyochukua mwezi mmoja yalifanyika chini ya usimamizl wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA).

Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala imesema majaribio hayo yalijikita katika maeneo mawili ambayo ni tuli (static) na mwendo (dynamic). Lengo la majaribio hayo ilikuwa ni kuangalia umadhubuti wa mabehewa treni inapokuwa kwenye mwendo.

Amesema wakati wa zoezi hilo LATRA imefanya kaguzi za mabehewa yote 264 kati ya hayo 200 yakiwa ni ya makasha (containers carriers) na 64 ni ya mizigo isiyofungwa (loose cargoes). 

“Aidha, LATRA imejiridhisha kuwa ubunifu wa mwendokasi (design speed} wa kilometa 120 kwa saa umefikiwa na kuthibitisha kuwa yamefanya vizuri katika mifumo yote muhimu ikiwemo breki na kwenye kona (curve),” amesema.

Katika hatua nyingine LATRA imesema itatoa ithibati kwa TRC, kama Sheria na Kanuni zinavyoeleza ili mabehewa haya yaanze kubeba na kusafirisha mizigo.

Kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 kati ya 1,430 yanayotengenezwa na kampuni ya CRRC ya China, ni kiashiria kuwa usafirishaji mizigo katika rell ya kiwango cha kimataifa (SGR) uko mbioni kuanza.

Leave a Reply