You are currently viewing Magu yawapa motisha wanafunzi bora, shule zilizong’ara 2024

Magu yawapa motisha wanafunzi bora, shule zilizong’ara 2024

HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu imegawa tuzo na zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 15 kwa shule za sekondari zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili, nne na sita kwa mwaka 2024.

Zawadi hizo ambazo ni vyeti, makombe na fedha tasilimu kwa walimu, zimelenga kuwapongeza na kuwapa motisha ya kuendelea kuwaanda vizuri wanafunzi kwa mitihani inayofuata.

Mbali na walimu wa shule hizo, pia wanafunzi waliofaulu vizuri masomo ya sayansi na hesabu nao pia wamepewa motisha ya fedha taslimu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika juzi Magu Mjini, Mkuu wa Wilaya Magu, Joshua Nassari ambaye alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri, Mohamed Ramadhani; Katibu Tawala, Jubilate Lawuo na Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga (CCM), amewapongeza walimu wa shule hizo kwa kuing’arisha wilaya hiyo kwenye sekta ya elimu nchini.

Pia amewataka wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo hayo kuendeleza jitihada zao katika masomo ili kufikia malengo yaliyojiwekea ikiwamo kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Aidha, Mkurugenzi wa wilaya hiyo amesema ufaulu wa kidato cha sita umepanda kwa 0.1% kutoka 99.9% kwa mwaka 2023 mpaka 100% kwa mwaka 2025 ambapo wanafunzi wote walifaulu kwa daraja la I-III hivyo hapakuwepo na daraja la IV wala 0.

Akifafanua zaisi kuhusu ufaulu huo, Afisa Elimu Sekondari Magu, Beatrice Balige amesema ufaulu wa mtihani wa upimaji kitaifa kwa kidato cha pili umepanda kwa 4.6% kutoka 82.1 % ya mwaka 2023 mpaka 86.7% kwa mwaka 2024.

“Ufaulu wa mtihani kitaifa  kidato cha nne umepanda kwa 9.5% kutoka 88% ya mwaka 2023 mpaka 97.5% kwa mwaka 2024.

Mshindi wa kwanza alipata Tshs 1,110,000, mshindi wa pili Tshs 900,000 na mshindi wa tatu tshs 690,000.

Leave a Reply