You are currently viewing Kicheko bei ya petroli, dizeli ikiendelea kushuka

Kicheko bei ya petroli, dizeli ikiendelea kushuka

BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeendelea kushuka baada ya bei za mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari mbalimbali kutangazwa kushuka kuanzia leo Jumatano, Desemba 4, 2024.

Taarifa ya Mamlaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kushuka kwa bei hizo, licha ya gharama za uagizaji mafuta kuongezeka kwa wastani wa asilimia 7.26 kwa petroli na kupungua kwa asilimia 12.80 kwa dizeli na wastani wa asilimia 7.10 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Ewura imesema hakuna mabadiliko katika Bandari ya Tanga, huku gharama zikiongezeka kwa wastani wa asilimia 15.67 kwa mafuta ya petroli. Pia hakuna mabadiliko kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa leo inaonyesha bei ya rejareja ya mafuta ya petroli yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam yameshuka kwa asilimia 1.55, dizeli ikishuka kwa asilimia 2.3 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.9.

Kutokana na hali hiyo lita moja itauzwa kwa Sh2,898 kutoka Sh2,943 iliyokuwapo Novemba 2024, dizeli ikifikia Sh2,779 kutoka Sh2,844 na mafuta ya taa yakifikia Sh2,831 kutoka Sh2,943.

Kwa Bandari ya Tanga, bei ya rejareja ya petroli itakuwa Sh2,905 mafuta ya dizeli yatakuwa Sh2,792 na mafuta ya taa yakiwa Sh2,877 kwa lita.

Hiyo ni pungufu ikilinganishwa na Sh2,948 ya lita moja ya petroli iliyouzwa Novemba 2024 na dizeli ilikiwa ikiuzwa kwa Sh2,855 na mafuta ya taa Sh2,989.

Kwa wanunuzi wa rejareja watakaotumia mafuta yanayopita Bandari ya Mtwara, watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,908 kutoka Sh3,015 iliyokuwapo Novemba mwaka huu, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,851 kutoka Sh2,916 na mafuta ya taa yatauzwa Sh2,903 kutoka Sh3,016.

Kutokana na suala hilo, Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa hizo kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022.

Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa hizo katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi, ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imeeleza taarifa hiyo ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk James Mwainyekule.

Kutofanya hivyo adhabu itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika, huku wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wakitakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), huku wanunuzi wakitakiwa kuhakikisha wanapata stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo zinatakiwa kuonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

“Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.

“Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli,” imeeleza taarifa hiyo.

Leave a Reply