KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, ametakiwa kujibu hoja za kada wao Lembrus Mchome inayowataka kutowatambua viongozi waliothibitishwa na Baraza Kuu la Chama hicho, kwa sababu wakati wa kikao hicho, akidi yao haikutumia kwa mujibu wa Katiba yao Ibara 6.2.2(b).
Katika barua yake, Mchome amesema hapakuwa na akidi kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ibara ya 6.2.2(b) na pia kulikuwa na watu waliokuwepo ukumbini ambao hawakuwa wajumbe na walioruhusiwa kupiga kura kama kanuni ya 7.3.2 ya Chadema inavyoelekeza.
Amesema kisheria viongozi wote walioteuliwa na Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu na kuthibitishwa na Baraza Kuu siyo halali.
Akitoa majibu ya sakata hilo, Mnyika aliandika kwa ufupi kuwa ajenda hiyo ni mahususi ili kuzima mpango wa ‘no reforms no election’ iliyoanzishwa na Chadema.
“Naomba kuweka wazi ukweli hapa, kuwa Katibu Mkuu aliandikiwa barua akiombwa ufafanuzi, na kwamba nafahamu jana Jumanne, alipewa ushauri kuwa asikurupuke kujibu bali awe na subira ili kutafuta majibu sahihi na yenye kutosheleza kama yatakuwepo.
Hii ni pamoja na kuzingatia ukweli kuwa Mchome alimjulisha Katibu Mkuu tangu Januari 25 mwaka 2025, kuwa atamwandikia ili kupata ufafanuzi juu ya masuala hayo mawili na ni kweli aliandika na mpaka jana alipoona barua yake mtandaoni alikuwa hajapokea majibu juu ya hoja zake kwa Katibu Mkuu.
“Sisi hapa Nairobi, tunafahamu kuwa Katibu Mkuu amekuwa kwenye shinikizo kubwa kukubaliana na mambo ambayo hakubaliani nayo na leo kathibitisha hilo, hasa kuhusu ajenda ya reforms alipokuwa anamjibu Mchome kuwa anahamisha au kukwamisha mjadala kuhusu reforms, ” alisema mwanachama wa Chadema aliyekuwa Nairobi, Kenya.
Sakata la Uchaguzi Mkuu wa Chadema ambalo limepatikana viongozi wake limeshika kasi ambapo taarifa za msuguano huo zimefika katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa lengo la kutoa ufumbuzi wa msuguano huo.