KAMATI ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya Ilungu pamoja na shule mpya ya sekondari Bundilya ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano wilayani Magu mkoani Mwanza katika ziara ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Simon Mpandalume kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo.

Akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi wa stendi Ilungu, Msimamizi wa mradi huo, Philipo Justine amesema ujenzi umefikia hatua ya boma na inayofuata ni kupaua boma hilo.
Amesema hadi sasa wametumia zaidi ya Sh milioni 73 kati ya Sh milioni 130 walizopatiwa huku mradi huo ukitarajiwa kutumia Sh milioni 165 fedha ambazo zinatolewa katika mapato ya ndani ya halmashauri.
Naye Msimamizi wa mradi wa shule mpya ya sekondari Bundilya iliyopo Kijiji cha Bundilya kata ya Kahangara wilayani Magu, James Ndega ameieleza kamati hiyo kwamba mradi huo ambao umefikia asilimia 95, unatarajiwa kuanza kusajili na wanafunzi 75 wa kidato cha kwanza.
Mbali na kutaja faida za mradi huo kuwa ni pamoja na kupunguza umbali mrefu wa wanafunzi kutembea, amesema ujenzi wake ambao ulianza Oktoba mwaka jana tayari umetumia kiasi cha Sh milioni 538.
Aidha, Afisa Elimu Sekondari Magu, Beatrice Balige amesema tayari walimu wanne wameletwa kwa ajili ya kuanza kufundisha katika shule hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika baada ya mwezi mmoja.

Akizungumzia miradi hiyo, Mpandalume mbali na kueleza kuridhishwa na ujenzi wake, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri kutangaza nafasi za ujenzi wa vibanda vya biashara kwa wananchi ili waanze kujenga katika eneo hilo la stendi kwa mujibu wa ramani ya mhandisi wa halmashauri.
Pia ametoa wito kwa viongozi kuhamasisha wazazi wawalete watoto wao wasome katika shule hiyo mpya hasa ikizingatiwa sasa hakutakuwa na visingizio vya wanafunzi kutembea umbali mrefu.