Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko ameipongeza Benki ya Exim kwa kuisaidia jamii kupitia Exim Cares ambayo imechangia vifaa vya matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 25.
Amesema mchango huo wa vifaa vya matibabu utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kahama.
Dk. Biteko ameeleza hayo jana Februari 25, 2025 Kahama mkoani Shinyanga wakati akizindua tawi la Benki ya Exim.
Amesema hatua kama hizi zinaonesha mshikamano wa sekta binafsi na Serikali katika kuboresha ustawi wa wananchi.

“Kahama ni kitovu kikubwa cha shughuli za kiuchumi, hasa sekta ya madini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Zaidi ya madini, mji huu pia ni maarufu katika sekta ya kilimo na biashara. Ni wazi kuwa ufanisi wa sekta hizi unategemea upatikanaji wa huduma za kifedha imara na zinazokidhi mahitaji ya wajasiriamali na wafanyabiashara.
“Hivyo, kwa kufungua tawi hili, Exim Benki inatoa fursa ya kipekee kwa wakazi wa Kahama kupata huduma za kifedha zinazoendana na shughuli zao za kiuchumi. Na kunaleta manufaa makubwa kwa jamii ya hapa Kahama, kwa wateja wengine wa benki na benki yenyewe kwa ujumla,” amesema.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza benki hiyo kwa hatua kubwa na kwa jitihada zake za kuleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi pamoja na kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.
Pia, amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za kifedha na kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kuwa ufunguzi wa tawi la benki hiyo ni kielelezo kuwa shughuli za uchumi ni nyingi na zitaendelea kuimarishwa.
Ameongeza kuwa Mkoa huo una matawi ya benki 11 ambayo yote pia yapo Kahama hivyo ni kiashiria kuwa Kahama ipo kibiashara na kuwa Mkoa huo uko tayari kushirikiana na benki hiyo.
Akitaja idadi ya benki zilizopo nchini amesema kwa sasa kuna benki 44, matawi zaidi ya 1000 na wakala wa huduma za kibenki zaidi ya 100,000 na hivyo ukuaji wa benki umeongezeka.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu amesema kuwa uzinduzi huo unathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kuleta suluhu ya masuala ya fedha na uwekezaji ambapo mwaka 1997 walizindua tawi la kwanza jijini Dar es salaam na kwa sasa taasisi hiyo ina wigo mpana wa kutoa huduma zake.
“Benki yetu imekuwa ikishirikiana mwa karibu na watu wa Kahama kwa shughuli mbalimbali ambapo tumewajulisha wakazi kuhusu huduma zetu na kuwa mshirika wa kudumu wa fedha,” amesema Bw. Matundu.
Aidha, amesema benki hiyo si tu imesaidia katika sekta ya afya bali hata elimu, ubunifu na kuwezesha wajasiriamali wanawake.
“ Tutaongeza ushiriki wa kifedha kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wanaotafuta suluhu ya kifedha kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika shughuli zao,” amebainisha Bw. Matundu.