You are currently viewing Dk. Mwasse: Stamico imeleta mapinduzi ya nishati ya kupikia kupitia Rafiki Briquette

Dk. Mwasse: Stamico imeleta mapinduzi ya nishati ya kupikia kupitia Rafiki Briquette

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse amesema nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes ni mkombozi katika mapambano dhidi ya nishati chafu na kwamba nishati hiyo ni mkombozi kwa Watanzania.

Dk. Mwasse amesema hayo Desemba 22, 2024 katika kilele cha wiki ya Nishati Safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes kilichofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke mkoani Dar es Salaam.

Amesema nishati hiyo ambayo ni mkaa unaotokana na makaa ya mawe umefanyiwa utafiti na vyuo vikuu mbalimbali na kubainika kuwa unakidhi mahitaji ya watanzania kwani ni rafiki na bidhaa hiyo ni bei nafuu.

Aidha, amesema STAMICO tayari wamesimika mitambo mikubwa ya kuzalisha mkaa huo kwenye Wilaya za Kisarawe mkoani Pwani na Kyela mkoani Mbeya kunakozalisha makaa ya mawe ambapo uzalishaji kwa sasa umefikia Tani 20,000.

Naye Mstahiki Meyaa wa Manispaa ya Temeke, Abdalla Mtinika ameipongeza STAMICO kwa kushiriki moja kwa moja kuzalisha Nishati safi na kuhamasisha matumizi yake ili kuleta mabadiliko kwa watanzania.

Amesema STAMICO imepiga hatua katika kufuata maelekezo ya Serikali ya kwamba ifikapo Disemba 31, 2024 Taasisi zinahudumia watu zaidi ya 100 ziache kutumia nishati chafu na kugeukia nishati safi.

Amesema kwa kuleta nishati hii STAMICO imefanya Mapinduzi yatakayoacha alama kwa kizazi kijacho kwa kuwa mazingira yatabaki kuwa salama kwa maisha ya watu.

Leave a Reply