You are currently viewing DC Kinondoni awalipia mabondia waliokosa pasipoti

DC Kinondoni awalipia mabondia waliokosa pasipoti

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule leo Ijumaa amegharamia malipo ya utengenezwaji wa paspoti kwa baadhi ya mabondia wa timu ya Taifa ya ngumi.

Mtambule amejitolea gharama hizo katika ofisi za uhamiaji akiambatana na mwenyekiti wa kamati ya wanawake ya shirikisho la ngumi la Taifa BFT, Aisha George  kwaajili ya mabondia hao waliokosa pasipoti na hawana uwezo kujilipia gaharama hizo.

Pia amewaomba wadau wengine kujitolea kwa chochote wanachoweza ili kuongeza nguvu kwenye timu hiyo ya taifa ya ngumi ya wanawake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya hiyo ameshukuru mkuu huyo wa wilaya Kinondoni kwa kuwasaidia mabondia hao wa kike wasiokua na hati hizo za kusafiria.

“Kwa kweli alichokifanya mkuu wa wilaya ni jambo kubwa sana ambalo halitasahaulika kuwasaidia wachezaji hawa kutimiza ndoto zao tunaomba viongozi wengine waige mfano huu wa kuunga mkono jitihada za  serikali ya za kukuza vipaji kwa wanamichezo ili watimize ndoto zao na kuleta chachu katika Tasnia ya michezo tunamhakikishia kumletea ushindi katika mashindano ya dunia,” amesema Aisha. 

Ikumbukwe kuanzia Januari 31 hadi Februari 2 mwaka huu yalifanyika mashindano ya mchezo wa ngumi kwa upande wa wanawake ya Samia Women Boxing Championship katika fukwe za Kawe jijini Dar es Salaam.

Lengo la mashindano hayo ilikuwa kutafuta mabondia watakaoingia kambini kwaajili ya kwenda katika mashindano ya ubingwa wa dunia yanayotarajiwa kufanyika nchini Serbia kuanzia Machi 6 hadi 17 mwaka huu.

Siku ya mwisho ya mashindano hayo mgeni rasmi alikua Mtambule na alitoa ahadi ya kuwasaidia mabondia hao na leo ametekeleza.

Leave a Reply