Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
Mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi katika Halmashauri ya Madaba Wilayani Songea Mkoani Ruvuma, unatarajiwa kuanza wiki ijayo kwa thamani ya Sh bilioni tano hadi kukamilika kwake.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Madaba, Abdul Manga mbele ya Mbunge wa Madaba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk. Joseph Mhagama, amesema mradi huo utagharimu Sh bilioni tano.
Manga amemshukuru mbunge huyo kwa kupambania maslahi ya wanamadaba na kuongeza haikuwa rahisi lakini ni jitihada zake zimemshawishi Rais Samia Suluhu Hassan kukubali stendi ijengwe.
Amesema stendi hiyo ya kisasa Madaba itafanana na Stendi ya Shule ya Tanga, Stendi ya Njombe n.k.
“Mradi huo utagharimu Bilioni 5 hadi kukamilika kwake, zimetolewa na Serikali ambapo milioni 205 zitaanza kutekeleza mradi huo utakaosimamiwa na Mhandisi wa Halmashauri ya Madaba, Jeremia Chambai.
Akifafanua kuhusu ujenzi huo, Chambai amesema eneo lina ekari tatu huku wakitarajia kuanza na ujenzi wa kibanda cha mlinzi, jengo la utawala, barabara za magari kuingilia pamoja na kutokea lakini pia wataweka taa pamoja na maeneo ya abiria kusubiria magari.
Aidha, kuelekea kuanza kwa ujenzi huo, Mbunge huyo ameagiza kifanyike kikao na wafanyabiashara wote waliojenga vibanda vya biashara katika eneo hilo la stendi ili wapewe ramani.
“Majengo yatakayosalia kwenye ramani hiyo wayaboreshe haraka ili yafanane na hadhi wanayoitaka wanamadaba na majengo yatakayoondolewa kulingana na ramani hiyo wafanyabiashara wapewe maelezo ili asiwepo wakupata hasara.
Naye Diwani wa Kata ya Litut, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba, Oraph Pili amemshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za ujenzi wa Stend hiyo huku akimshukuru pia Mbunge wa Madaba kufanikisha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa stendi ya kisasa.