Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited, David Mulokozi amenunua ndege binafsi aina ya Helkopta ambayo ameitumia kutua kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Stadium uliopo Babati mkoani Manyara huku akiwa ameambatana na familia yake.
Mulokozi anaingia miongoni mwa Watanzania wachache wanaomiliki ndege binafsi ambapo amesema kuwa kampuni yake imekua ikikua siku hadi siku na kuonyesha vitu vya tofauti.
“Hakuna Mtu alitegemea kuwa Manyara kunaweza kuwa na helkopta ni mambo mengi yanaanza, wafanyabiashara wengi wanajifunza, kila mtu anaruhusiwa kumiliki chombo hichi inawezekana,” amesema Mulokozi.
Amesema kuwa ndege hiyo itasaidia katika utoaji wa huduma katika kampuni yake inayojihusisha na uzalishaji wa vinywaji changamshi.
Mulokozi ameiomba Serikali ijenge kiwanja cha ndege ili ndege nyingi zaidi ziweze kutua mkoani Manyara.
Kwa upande wao wakazi wa mkoa wa Manyara waliofika na kushuhudia helkopta hiyo ikitua akiwemo Melkiori Enyasi anaelezea furaha yake baada ya kuona ndege binafsi ya kwanza ya mkazi wa mkoa wa Manyara ikitua katika ardhi nyumbani.
Enyasi amempongeza Mulokozi kwa kununua ndege binafsi itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi .