Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amefika eneo ilipotokea ajali ya basi la abiria lenye namba za usajili T857 DHW, katika eneo la Kabukome katika Kata ya Nyarubango wilayani Biharamulo mkoani Kagera na kuwajulia hali majeruhi wanaoendelea kupewa matibabu katika hospitali teule ya Biharamulo, tarehe 21 Disemba 2024.
Basi hilo liliokuwa linafanya safari kutoka Kigoma kwenda Bukoba wakati liliposimama kushusha abiria ambae alipitilizwa kwenye kituo, lilishindwa kuondoka na kuanza kurudi nyuma kisha kuacha njia na kupinduka.
Ajali hiyo imesababisha vifo vya abiria 11 na majeruhi 16 ambapo Majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali teule ya Biharamulo mkoani Kagera.
Akizungumza baada ya kutembelea majeruhi, Waziri Bashungwa ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wote walioguswa na ajali hiyo na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwaombea majeruhi wapone haraka.
“Nitumie nafasi hii kuombea raho za marehemu ambao tumewapoteza katika ajali ambayo imetokea hapa Biharamulo, tumepoteza ndugu zetu 11, wametangulia mbele za haki” amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara imeanza kufanyia kazi Maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya marekebisho ya kuwa na mfumo wa leseni za udereva ili kuwapunguzia alama madereva wanafanya makosa yenye kuhatarisha usalama barabarani ambazo zitapelekea kuwafungia leseni.
Kwa Upande wake, Mganga mkuu wa Hospitali teule ya Biharamulo, Gresmus Sebuyoya ameeleza kwa majeruhi 26 wameruhusiwa na wengine 16 wanaendelea na matibabu na ungalizi wa karibu.
“Tumebaki na watoto wanne ambao wanaendelea vizuri, wanaume tunao sita, vifo tulikuwa navyo kumi na moja, wanawake watano, wanaume wanne na watoto wawili” ameeleza Dk. Gresmus.