You are currently viewing Bashungwa aridhishwa na utendaji kituo cha kutengeneza vitambulisho vya Taifa

Bashungwa aridhishwa na utendaji kituo cha kutengeneza vitambulisho vya Taifa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Innocwent Bashungwa ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa kituo cha uchakataji taarifa za utambulisho wa Taifa cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Akizindua magari mapya nane aina ya Landcruiser hardtop  kati ya 20 yaliyoagizwa yakiwa na thamani ya Sh bilioni 2.2 Jijini Dar es Salaam jana Jumanne, magari 12 yaliyosalia yatawasili hivi hivi karibuni.

Waziri Bashungwa alielezea kufurahishwa utendaji kazi wa NIDA kwa sasa na kusema waendelee na spidi hiyo hiyo.

“Licha ya magari hayo 20, nimeambiwa mmetenga shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari mengine 10 katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2024/2025,” alisema Bashungwa.

Bashungwa kabla ya kuzindua magari hayo katika ofisi za makao makuu hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam, alitembelea ofisi mbalimbali za Mamlaka hiyo ikiwemo ya Kibaha Mkoani Pwani.

“Nimefurahishwa na utendaji kazi wa kituo kwa sasa, na pia kama Serikali tutahakikisha kuwa changmaoto  mbalimbali za usafiri zitatatuliwa  haraka iwezekanavyo,” alisema.

Pamoja na hayo Bashungwa aliwataka vijana kuchangamkia fursa   ya kujiandikisha  kwa hiyari katika mamlaka hiyo ili kuwa na vigezo vitakavyowawezesha kujiunga na vyuo vikuu, kupata mikopo na fursa  mbalimbali za kazi za ndani na nje ya nchi.

“Natoa rai kwa NIDA kuhakikisha  ndani ya miezi miwili mnasambaza vitambulisho vyote vilivyotengenezwa kwa wahusika ili waweze kuvitumia kwa matumizi yao mbalimbali” alisisitiza Bashungwa.

Aidha Bashungwa alimshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Tsh. 42.5 bilioni kwa ajili ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika mwaka huu wa fedha wa 2024/2025.

“Kuhusu changamoto za kifedha zinazoikabili NIDA nitazungumza na hazina ili kuona namna bora ya kuzitatua na kufanikisha zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wananchi”  alisema Bashungwa

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Deusdedit Buberwa, aliishukuru Serikali kwa kukabidhi magari hayo na kuahidi kuwa yatatunzwa na yatatumika kwa kazi iliyokusudiwa.

“Magari haya yatatusaidia sana sisi kwa ajili ya kazi kubwa mbili kama vile kusajili wananchi pamoja na kusambaza vitambulisho kama alivyosema Mheshimiwa Waziri hivi punde” alisema Buberwa.

Aliongeza kuwa jiografia ya Tanzania inatofautiana sana kutoka sehemu moja mpaka nyingine hivyo magari hayo yatarahisisha kazio yao kwa kiasi kikubwa na kuweza kutimiza adhma ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata kitambulisho chake cha Taifa.

“Kwa upande wa vitambulisho mpaka Novemba 2024, tulikuwa tumekwisha sajili jumla ya watu zaidi ya milioni 25, kati ya hao tayari wananchi milioni 21 wamekwishapatiwa namba za utambulisho” alibainisha Buberwa.

Leave a Reply