You are currently viewing Balozi Ulanga aitabiria makubwa NFRA

Balozi Ulanga aitabiria makubwa NFRA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula nchini (NFRA) Balozi John Ulanga ameitabiria mafanikio makubwa taasisi hiyo kutokana na jitihada madhubuti zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijii Arusha mwishoni wa juma lililopita mara baada ya kikao cha bodi hiyo kilichodumu kwa siku mbili, Balozi Ulanga alisema jitihada za Rais Samia  kwa kushirikiana na NFRA zimewezesha kuhakikisha kila mwaka nchi inakuwa na akiba ya kutosha ya chakula inatekelezeka.

“Maono na  ndoto za Mheshimiwa Rais ni kwamba mpaka kufikia mwaka 2030 tunataka kuwa na ya mageuzi ya sekta ya kilimo sio tu kwa manufaa ya nchi yetu lakini pia kwa manufaa ya bara zima la Afrika” alibainisha Balozi Ulanga.

Ulanga alisema wao kama Mamlaka ya Uhifadhi wa Chakula wana jukumu kubwa la kutekeleza maono ya Rais ya kuhakikisha wanakuwa na hifadhi ya kutosha ya chakula kwa matumizi ya ndani ya nchi na kingine  kuuzia nchi ambazo  wameingia nazo mkataba.

Balozi Ulanga alisema kwa sasa wana mikataba na nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lakini pia shirika la kimataifa la WFP.  Mikataba hiyo yote ni ya  kuuza chakula kuanzia tani laki moja hadi laki tatu, alisema pia wana mpango wa kuongeza masoko kwa nchi nyingine za Afrika.

“Kama mnavyokumbuka Mheshimiwa Rais alisema angependa Tanzania iwe ndiyo hifadhi ya chakula ya bara la Afrika na sisi ndiyo mamlaka ya uhifadhi wa chakula, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha ndoto na maono ya Mheshimiwa Rais yanafanikiwa” alibainisha Balozi Ulanga.

Balozi Ulanga aliweka wazi  kuwa mojawapo ya malengo yao mpaka ifikapo mwaka 2030 ni kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani milioni tatu za nafaka, ambapo ni mara nne ya uwezo wao wa sasa, pia alisema tayari wako katika mipango mikakati ya kuhakikisha wanapata vyanzo mbalimbali vya fedha chini ya baraka za Mheshimiwa Rais ili kuweza kufikia malengo hayo.

Aidha, Balozi Ulanga alisisitiza kwamba lengo lao sio tu kuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka, lakini pia kuwa na uwezo wa kuingia mikataba na nchi mbalimbali katika bara la Afrika hasa kwa zile  zinazokuwa na upungufu wa chakula ili kuweze kukidhi mahitaji yao ya chakula, na ndiyo maono   ya Mheshimiwa Rais wa kuwa Tanzania iweze kuwa hifadhi ya chakula ya bara la Afrika.

Hata hivyo, Balozi Ulanga alisema kuelekea mwaka 2030 wanatengeneza mpango mkakati utakaoainisha vipaombele vyote kwa ujumla wake ambavyo vitakuwa na lengo la kuongeza uwezo wa mamlaka wa kuhifadhi shehena ya kutosha.

“Katika kipindi hiki cha miaka minne ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga miundombinu bora ya kuhifadhia chakula hususani mahindi” alisema Balozi Ulanga.

Balozi Ulanga alisema kuwa wakulima wamepata faida nzuri hasa kwa wale waliouza mazao yao kwa NFRA na wamepata malipo mazuri tofauti na wangeuza kwa wafanyabiashara wengine wa kawaida.

“Mheshimiwa Rais ameendelea kutujali na kutuunga mkono  kwa kutupa kibali cha kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha hapa nchini, lakini pia kuongeza kiwango cha bajeti  tulichokuwa tunakipata kutoka kwenye wizara ya fedha kwani kimetuongezea uwezo wa kununua shehena zaidi” alisema Balozi Ulanga.

Balozi Ulanga alisema katika mwaka uliopita wa fedha wa 2024/2025 waliweza knunua zaidi ya tani laki nne za mahindi na nafaka nyingine kutoka kwa wakulima hapa nchini.

Hiyo pia imetuwezesha NFRA kutoa bei nzuri sana kwa wakulima wamepata bei nzuri sana kutoka kwetu tofauti na bei ambayo wanawauzia wafanyabiashara wengine kwa hiyo hiyo imeweza kumnufaisha mkulima moja kwa moja.

Leave a Reply