Na Mwandishi Wetu, Tabora
Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali (mstaafu) Fred Mwesigye amevutiwa na utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP), akisema kukamilika kwa mradi huo utakuza uchumi wa mataifa hayo mawili na kutoa ajira kwa wananchi wake.
Akizungumza wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania na Uganda kwa ajili ya kujionea maendeleo ya mradi huu katika kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora, Balozi Mwesigye amesema mradi huu ni mkubwa kupata kutokea katika Afrika, ambao utaacha alama kubwa katika mataifa haya, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakishirikiana katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Amesema wameamua kutembelea katika kiwanda hicho cha Sojo kwa sababu ni eneo muhimu katika utekelezaji wa mradi huu, akimwakilisha Rais wa Uganda Yoweri Museveni ili kujionea kazi zinavyofanyika.
“Mabomba yote yanayotoka nje ya nchi yanaletwa hapa na kuwekewa koti juu ili kusaidia usafirishaji wa mafuta ghafi ( mazito) yanayotoka Uganda kwenda pwani ya Tanga na baadae kusafirishwa nje ya nchi.
” Yatafukiwa aridhini kuanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga yakiwa na umbali wa kilomita 1443, hivyo ni eneo muhimu sana katika utekelezaji wa mradi huu,” amesema wakati akiongea na waandishi wa habari.
Akielezea kuhusu faida za utekelezaji wa mradi huu, Balozi Mwesigye amesema uchumi wa nchi hizi utakuwa kwa kiasi kikubwa kupitia tozo mbalimbali za kodi na ajira zinazotolewa kwa makampuni ya ndani ya wazawa kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mradi na ajira zinazotolewa kwa wataalamu wazawa wakiwemo watu wasio na ujuzi wanaoishi kando kando ya bomba hili linapopita katika mikoa nane hapa nchini.
Amesema hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huu ni kubwa na ya kujivunia na hii ni ishara ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa mpaka sasa.
“Nitafurahi kuwaona wabunge wa Uganda na Tanzania kwa pamoja wakitembelea pia eneo hili ambalo mabomba yote ya mradi yanafikia hapa, ili waone hatua iliyofikiwa mpaka sasa katika utekelezaji wake.
“Nilikuwa hapa Sojo miaka miwili iliyopita wakati mradi huu ukiwa katika hatua za awali na leo hii nimeshuhudia maendeleo makubwa, ikiwemo sehemu moja ya kiwanda ikianza uzalishaji ambapo mabomba yote yatakayosafirishwa kwenda sehemu mbalimbali ikiwemo Uganda,” amesema.
Akiongelea wanaobeza utekelezaji wa mradi huu kuwa una athari za kijamii na kimazingira, Balozi Mwesigye amesema kuwa hizo ni propaganda ambazo zinarudisha nyuma maendeleo ya nchi hizi mbili.
“Hatuwezi kuwazuia kusema, wacha wasema, ila sisi tunaendelea na mradi huu kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa uchumi na wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini Uganda (PAU), Ernest Rubondo amesema kuwa amefurahishwa sana kuona maendeleo na hatua ya mradi huu yaliyofikiwa mpaka sasa.
Amesema mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali na utakuwa na faida kubwa kwa maendeleo ya nchi hizi.
“Tunaushukuru sana mradi wa EACOP kwa kuandaa ziara hii ambayo tumejifunza mambo mengi sana,” amesema.
“Tumejiona teknolojia kubwa inayotumika hapa Sojo katika kuyatengeneza mabomba haya yatakayosafirisha mafuta ghafi na sehemu kubwa ya mafundi kwa upande wa Tanzania ni wazawa ambao mwisho wa siku watabakiwa na ujuzi huu kwa ajili ya miradi mingine ijayo.
“Hii ni faida kubwa kwa Watanzania kwa sababu sehemu kubwa ya utekelezaji wa mradi huu unafanyika hapa nchini na sehemu ndogo nchini Uganda,”, amesema Rubondo na kuongeza;
“Kiukweli tumejifunza mengi kupitia utekelezaji wa mradi huu hapa Tanzania na sisi kwa upande wa Uganda tunaendelea vizuri ili kuhakikisha umalizika na kuanza kazi,”.
“Lakini pia tumefurahi sana kuwaona wenzetu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji ( Ewura ) kwa upande wa Tanzania katika ziara hii, ikionyesha ni kwa namna gani pande zote mbili tunashirikiana kwa ukaribu na kubadilishana uzoefu kupitia mradi huu,”
“Ushirikiano huu ni kielelezo cha urafiki wa miaka mingi kati ya Tanzania na Uganda kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake,” amesema.
Akiongea wakati wa kuwakaribisha wageni hao katika kiwanda hicho kabla ya kutembelea na kujionea maeneo mbalimbali ya uzalishaji, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP anayemaliza muda wake Martin Tiffen amesema mradi huu umezingatia hatua zote muhimu kulingana na mikataba wa kimataifa, ikiwemo kuwalipa fidia walioguswa.
“Tunaendelea na utekelezaji wa maeneo mbalimbali ikiwemo kazi ya usafirishaji mabomba kuja hapa Sojo na kuwekewa vifaa maalum kwa ajili ya kusaidia usafirishaji wa mafuta hayo,” amesema Tiffen.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Mafuta kutoka Ewura Gerald Maganga amesema wakiwa kama wasimamizi wa nishati hapa nchini wamefurahishwa na maendeleo ya mradi huo na kuona kiwanda cha Sojo kinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
“Hii itasaidia kwa haraka kusambaza mabomba haya katika maeneo yote unakopita mkuza kwa ajili ya kazi ya ufukiaji,” amesema.
Mradi wa bomba la ghafi la Afrika Mashariki unahusisha wanahisa wanne, ambapo TotalEnergies inamili asilimia 62, Mamlaka za nishati na mafuta nchini Tanzania na Uganda zikimiliki asilimia 15 kila moja na ile ya China ikimiliki asilimia nane.