You are currently viewing EACOP waahidi kushirikiana zaidi na vyombo vya habari

EACOP waahidi kushirikiana zaidi na vyombo vya habari

UONGOZI wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrka ya Mashariki (EACOP) umesema kuwa unatambua umuhimu wa vyombo vya habari katka kuuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali yanayogusa jamii ikiwemo mradi huo na kuahidi kuendelea kufanya kazi pamoja na vyombo hivyo katika kutoa taarifa za hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati ziara ya kutembelea vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mradi huo upande wa Tanzania, Catherine Mbatia amesema kuwa wataendelea kutoa elimu kwa waandishi wa habari kupitia njia mbalimbali, ikiwemo kutembelea vyumba vya habari ya magazeti, vituo vya redio na televisheni sambamba na kuandaa semina na kukutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa juu ya maendeleo ya mradi huo.

“Mahusiano yetu na vyombo vya habari ni muhimu sana ili wananchi waendelee kupata taarifa juu ya maendeleo ya mradi huu,”alisema na kuongeza kuwa wakati mwingine wananchi wanapenda kujua hatua za utekelezaji wa mradi huu.

Amesema mbali ya kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia pia waandishi wa habari wanatumiwa kama daraja muhimu la kuwapatia taarifa za mradi huu.

Amesema wananchi wanahitaji matokeo mbalimbali za mradi ikiwemo faida za kiuchumi kwa taifa.

Hivyo, amesema wananchi wanahitaji kupewa taarifa sahihi kulinganisha na kila hatua ya mradi huo, ambao utahusika kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga na baadae kusafirishwa nje ya nchi.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi, Mbatia amesema kuwa unaendelea vizuri na matarajio ni kumalizika kwa wakati.

Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo ufukiwaji wa mabomba ardhini yatakayosaidia kusafirisha mafuta ghafi kutoka kijiji cha Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Bomba hilo lina urefu wa kilomita 1,443, ambapo kati ya hizo, kilomita 1,147 zipo nchini Tanzania na kilomita nyingine 296 zipo nchini Uganda.

Wanahisa wa mradi huu ni kampuni ya TotalEnergies inayomiliki asilimia 62, mashirika ya kusimamia Nishati nchini Tanzania (TPDC) na UNOC ya Uganda yanamiliki hisa asilimia 15 kila moja wakati lile la China (CNOOC) linamiliki hisa nane.

Leave a Reply