NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Katiba na Sheria (MoCLA), imeishukuru Benki ya NMB kwa kukubali kuendesha mafunzo ya kukijengea uwezo Kituo cha Huduma kwa wateja cha wizara hiyo, kilichotembelea Kituo cha Huduma kwa Wateja NMB ‘NMB Contact Center,’ kujifunza mifumo ya kupokea taarifa, malalamiko, kero na changamoto za wateja na kuzitatua.
Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Lawrence Kabigi, aliyeongoza masafara wa watumishi wa kituo hicho, wafanyakazi wa MoCLA na Wanasheria wa Serikali, alipokuwa akitoa neno la shukrani kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna baada ya kukamilisha mafunzo yao.
Kabigi alibainisha kuwa, siku mbili za mafunzo yao NMB, hususani katika Kituo cha Huduma kwa Wateja ‘NMB Contact Center,’ yeye na washiriki wengine kutoka MoCLA wamejifunza mengi, ikiwemo namna kituo hicho na taasisi nzima inavyotoa huduma tangu kupokea malalamiko na kero za wateja wao na kuyashughulikia kwa utaratibu wa kisasa zaidi.

“Tulikuja hapa pia kuona tunatofautiana vipi katika teknolojia kwenye kushughulikia changamoto za wateja wenu, tumejionea namna mlivyotengeneza mifumo bora, sahihi na ya kisasa inayoshughulikia changamoto. Mifumo mizuri ambayo haimhitaji tu mfanyakazi kujibu, bali mifumo yenyewe inajibu na kuleta suluhishi za kimahitaji.
“Na sisi tunaangalia namna ya kufikia ufanisi wenu katika kuhudumia wananchi wanaosubiri kutoka kwetu ufumbuzi wa changamoto zao, tukiamini kwamba tunapopambana kumaliza kero na changamoto za wananchi bila kutumia muda wao, tuNawapa wigo mpana wa kuendelea kuwajibika na uzalishaji mwingine na kukuza pato lao na la taifa kwa ujumla.
“Mwananchi ambaye tutamsaidia kumaliza changamoto zake, hata asipotulipa tutakuwa tumempa muda wa kufanya mambo mengine na kwa mantiki hiyo ataweza kulipa kodi serikalini.
“Kimsingi sisi hatubagui malalamiko ya wananchi, tunayapokea yote na yaliyo ndani ya wizara yetu yanatatuliwa, na yale ya wizara ama idara za serikali, taasisi za umma na binafsi tunayapeleka na tunafuatilia ufumbuzi wake.
“Tunashukuru kwa mafunzo haya, ambayo si tu yalikuwa ya nadharia, bali kwa vitendo kupitia wataalam mahiri na wabobevu wanaohudumu kwenye vitengo mbalimbali bila kuathiri usiri wa taarifa za wateja wenu,” alisema Kabigi na kutaka mashirikiano baina ya MoCLA yaendelee kwa ustawi wa maisha ya Watanzania wa kada zote.
Kwa upande wake, Bi. Zaipuna aliishukuru MoCLA kwa kuichagua NMB katika kuwajengea uwezo Watumishi wa Kituo chao na kusema wizara imechagua mshirika sahihi katika kujifunza Huduma kwa Wateja, hasa ikizingatiwa kuwa NMB Imefanya mapinduzi makubwa ya kimifumo na kiteknolojia kuhakikisha huduma zao ni za vuiwango vya juu.
“NMB ni Benki ya Serikali, ndio maana tunaamini mambo mengi tutayafanya pamoja na kwa uelewano. Hapa mmefika mahali sahihi, sisi mwaka 2020 tuliona tuje na Mpango Mkakati wa ‘kui-transform’ benki, tukaona ulazima wa kufanya uwekezaji. Tukafanya uwekezaji kwenye rasilimali watu na mazingira yao.
Baada ya hapo eneo lingine ambalo tuliliona bila uwekezaji ‘hatutoboi’, ni teknolojia. NMB imewekeza kwa kiasi kikubwa sana katika teknlojia, tumewekeza kwenye ‘data center,’ tumewekeza kwenye ‘contact center’ na uwekezaji huu ndio unaotuwezesha sasa kufanya bunifu hizi zenye tija kwa benki.
“Tukawekeza pia kwenye Utawala Bora na sasa kila Mtanzania anajua kuwa NMB ni benki ya aina gani, ndio maana tumeifikisha benki mahali ambapo inatajwa sio tu Mlipa Kodi Mkubwa na Bora Zaidi Tanzania, bali pia Mlipa Kodi Anayefuata Kanuni na Sheria za Ulipaji Kodi,” alifafanua Bi. Zaipuna.
Alibainisha kuwa, Mwaka jana 2024 baada ya kuona tayari benki imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye rasilimali watu, teknolojia, utawala bora, pamoja na ‘performance,’ wakaona kitu pekee kilichobaki kuwatofautisha na taasisi zingine za kifedha, uwekezaji kwenye Huduma kwa Wateja, ambayo sasa imekuwa mfano kwa taasisi nyingi.
“Nasisistiza kuwa MoCLA mmechagua mshirika sahihi, twendeni pamoja, tutakua pamoja, tutasaidia utatuzi wa changamoto za wananchi wetu pamoja. Tuna majukwaa mengi yatakayotuwezesha kumfikia Mtanzania hadi wa chini, ikiwemo Mpango wa Huduma za Kibenki Vijijini, ambao mwaka jana ulifikia vijiji 1,300 ambavyo havuikuwahi kufikiwa na huduma za kibenki.
“Hivyo vijiji 1,300 ambavyo havikuwahi kufikiwa na huduma za kibenki, huko tumeacha mawakala kuanzia wawili na kuendelea katika kila kijiji, ambapo takwimu zetu zinaonesha tumefungua akaunti Milioni 1.5 kwa mwaka jana, ambako tulitembelea vijiji vingi na Jukwaa letu la Elimu ya Fedha la NMB Kijiji Day,” alibainisha Bi. Zaipuna.
Aidha, wakati wa ufunguzi wa ziara hiyo ya mafunzo juzi Aprili 23, Kabigi alisema kituo chake kilichozinduliwa Septemba 2024, kikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Kitaifa ya Huduma za Kisheria ya Mama Samia, kilivutiwa na mafanikio na ufanisi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja NMB ‘NMB Contact Center,’ hivyo kuwasukuma kufanya ziara hiyo.
Alibainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria iko imara katika kusimamia jukumu la kutetea haki za wananchi walilopewa na Serikali kupitia Hati Idhini kwa Tangazo la Serikali Namba 619A la Agosti 30, 2023, ambalo linawataka pamoja na mambo mengine, kuhakikisha wanashughulikia haki na upatikanaji wa haki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Biashara za Serikali wa NMB, Bi. Vicky Bishubo, alimshukuru Katibu Mkuu MoCLA, Eliakim Maswi, ambaye aliratibu ziara Kituo cha Huduma kwa Mteja cha wizara hiyo, lengo likiwa kukijengea uwezo na kuomba muendelezo wa mashirikiano mema, ya dhati na ya kimkakati katika kuhudumia jamii ya Watanzania.
“Kupitia ziara hii, sisi NMB tunaahidi kuendelea kuwa Wadau Vinara wa Kimkakati wa Serikali katika kutoa huduma bora kwa Watanzania. Tunaamini kwamba siku mbili za ziara hapa, zimekuwa na faida kubwa kwao, lakini pia kwetu sisi kwa sababu nasi pia tumejifunza kutoka kwao,” alisisitiza Bi. Vicky Bishubo.