Mwenyekiti wa Halmaahauri ya Wilaya ya Magu, Simon Mpandalume amesema katika kipindi cha miaka mitano Halmashauri hiyo imeongeza makusanyo ya mapato ya ndani kutoka Sh bilioni 2.4 hadi bilioni 5.2.

Mpandalume ameyasema hayo leo Alhamisi wakati wa mkutano wa baraza la madiwani ambao pamoja na mambo mengine amewapongeza madiwani, Mkurugenzi Mtendaji na watumishi wa halmashauri kwa ushirikiano ambao umewezesha kupandisha wigo wa makusanyo ya mapato ya ndani.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano Halmashauri ya Wilaya ya Magu imefungua shule mpya 24 kwa kutumia mapato ya ndani.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari ametoa wito kwa viongozi wanaohusika na usimamizi wa miradi kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili miradi hiyo isaidie wananchi.
Pia ametoa pongezi kwa wadau na wananchi wa Wilaya ya Magu kuridhia mchakato wa maombi ya kuligawa jimbo la Magu amesisitiza kuwa mchakato huo ukikamilika utachochea maendeleo katika Wilaya ya Magu.
Naye mwakilishi wa katibu tawala wa mkoa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kupata hati isiyo na mashaka kwenye ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali ( CAG)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani ametoa wito wananchi ambao hawakupata fursa ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kujitokeza kushiriki uboreshaji wa daftari hilo awamu ya pili linalotarajiwa Kuanza Mei 1-7 , 2025.