You are currently viewing NMB yabuni mfumo wa kidijitali wa kusimamia matumizi ya fedha za umma

NMB yabuni mfumo wa kidijitali wa kusimamia matumizi ya fedha za umma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Benki ya NMB, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imebuni na kuzindua mfumo wa kisasa wa kidijitali wenye lengo la kusaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha za umma.

Mfumo huu wa benki mtandao, ambao ni wa kwanza wa aina yake nchini, ulizinduliwa rasmi jana (Alhamisi) jijini Dodoma na kupokelewa kwa shangwe na wadau mbalimbali, wakiwemo Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri 184 nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Biashara ya Serikali, Bi Vicky Bishubo, alibainisha kuwa mfumo huu ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya NMB na Serikali katika kuboresha huduma za kifedha, kuongeza uwazi kiutendaji, na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.

“Hatua hii ni sehemu ya jitihada za NMB na TAMISEMI katika kuleta mageuzi ya kidijitali ndani ya sekta ya umma. Lengo ni kuhakikisha mifumo ya kifedha inakwenda sambamba na teknolojia za kisasa kwa manufaa ya taifa,” alisema Bi Bishubo.

Miongoni mwa faida za uwekezaji huu ni utaratibu mzima kuongeza ufanisi kwa kurahisisha usimamizi wa fedha za umma, kudhibiti upotevu wa fedha kwa kupunguza mianya ya upotevu wa fedha za umma, na kuimarisha uwajibikaji kwani mfumo unaruhusu ukaguzi wa fedha kufanyika kwa wepesi.

Bi Bishumo alisema faida nyingine kubwa ni kuongeza uwazi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa kusaidia kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya fedha.

Aidha, alisisitiza kuwa huduma hii ni muendelezo wa dhamira ya NMB kushirikiana na Serikali kuhakikisha teknolojia za kidijitali zinaboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na kusaidia kujenga uchumi wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Bi Bishubo, mfumo huu wa kidijitali utawezesha TAMISEMI kufuatilia kwa karibu matumizi ya rasilimali za Serikali kwa taasisi zake. Pia utapunguza haja ya kusafiri kwenda benki kwa ajili ya kupata taarifa za akaunti, kwani taarifa zote zitapatikana kwa mtandao.

“Mfumo huu sio tu kwamba utarahisisha upatikanaji wa taarifa za akaunti, bali pia utawezesha malipo mbalimbali kwa njia ya mtandao, ikiwa ni pamoja na malipo ya posho na huduma mbalimbali kwa watumishi wa Serikali za Mitaa,” alisema.

NMB ilianzisha mfumo huu baada ya kubaini changamoto zinazowakabili halmashauri nyingi, shule, vituo vya afya, vijiji, na mitaa katika kupata huduma za kifedha za kidijitali.

Uzinduzi wake unafuatia majaribio ya miezi tisa ambayo yalionesha matokeo chanya, huku ukionesha uwezo mkubwa wa kubadilisha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma nchini.

Aidha, NMB inaendelea kuwa mshirika wa kimkakati wa Serikali katika ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mtandao, kupitia mifumo ya kisasa.

Mfumo huu pia umeunganishwa na Mfumo wa Serikali wa Malipo (MUSE), ambao umeongeza ufanisi katika malipo ya mishahara na huduma mbalimbali serikalini.

Kutambulishwa kwa huduma mpya ya benki mtandao kuliendana pia na uzinduzi wa semina ya mafunzo ya siku mbili kuhusu teknolojia hii kwa wahasibu na wakaguzi kutoka halmashauri 184 za serikali za mitaa nchi nzima.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Bw. Adolf Ndunguru, ambaye aliipongeza Benki ya NMB kwa uwekezaji wake mkubwa katika mifumo ya kielektroniki na kwa juhudi zake za kusimamia nidhamu katika fedha za umma.

Kwa mujibu wa Bw. Ndunguru, suluhisho hili jipya ni hatua muhimu katika kuboresha usimamizi wa fedha katika ngazi ya serikali za mitaa, na pia linachagiza ufanisi na uwazi katika sekta ya umma kwa jumla.

Aliongeza kuwa tangu TAMISEMI ilipoanzisha jitihada za huduma mtandaoni mwaka 2017, kumekuwepo na manufaa makubwa, ikiwemo kupunguza matumizi ya karatasi, kupoteza muda, na rasilimali fedha.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Rais, Bi. Angelista Kihaga, alisisitiza kuwa utekelezaji wa sera ya benki mtandao ni jambo lisilopingika katika zama hizi ambapo mageuzi ya kidijitali katika sekta ya umma ni suala la kufa na kupona.

Leave a Reply