You are currently viewing Besigye akimbizwa hospitalini
Kizza Besigye

Besigye akimbizwa hospitalini

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye ambaye alianza mgomo wa kula wiki iliyopita amekimbizwa hospitali jana jioni baada ya hali ya afya kuzorota.

Hayo yameelezwa na mbunge mmoja mwenye mafangumano na Besigye na kuripotiwa pia na kituo kimoja cha televisheni nchini humo.

Mbunge  Francis Mwijukye ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba Besigye amepelekwa kwenye kliniki ya Bugolobi chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya dola.

Kituo cha televisheni cha NTV nacho kimeripoti kuwa Beisgye amekimbizwa hospitali na kwamba kuna ulinzi mkali kwenye eneo anakotibiwa.

Mpinzani huyo mkubwa wa kisiasa na mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni amekuwa kizuizini kwenye jela yenye ulinzi mkali mjini Kampala tangu November mwaka jana.

Wanasheria wake wanasema “alitekwa nyara” nchi jirani ya Kenya na kusafirishwa kwa mabavu hadi nchini Uganda na kufunguliwa mashtaka kwenye mahakama ya kijeshi yanayojumuisha umiliki wa silaha kinyume cha sheria.

Alianza mgomo wa kula kushinikiza kesi yake ihamishwe kwenda mahakama ya kiraia baada ya mahakama ya juu ya Uganda kutoa uamuzi mwezi uliopita kuwa raia hawawezi kushtakiwa chini ya mahakama za kijeshi.

Waziri wa Mawasiliano wa Uganda Chris Baryomunsi alisema jana kwamba serikali tayari inaharakisha mchakato wa kuhamisha kesi hiyo ya Besigye kwenda mahakama ya kiraia.

Leave a Reply