You are currently viewing RC Chalamila atangaza uuzaji viwanja 2,274 Mabwepande- Kinondoni

RC Chalamila atangaza uuzaji viwanja 2,274 Mabwepande- Kinondoni

Kufuatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka waliovamia na kujenga kwenye eneo linalomilikiwa na shirika la maendeleo Dar es Salaam (DDC) lililopo Mabwepande kuuziwa viwanja kwa gharama nafuu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila kwa kushirikiana na shirika hilo pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya kinondoni ametangaza rasmi rasmi kuanza  kuuza viwanja katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 8, 2025 eneo la Mabwepande akiwa ameambatana Katibu Tawala wa Mkoa Dkt Toba Nguvila, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, viongozi wa DDC pamoja na wataalamu wa ardhi kutoka Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni RC Chalamila amesema eneo hilo lenye viwanja zaidi ya 2274 vyenye ukubwa tofauti tofauti ambavyo baadhi vilivamiwa na vingine havijavamiwa vitaanza kuuzwa rasmi. 

Aidha, RC Chalamila amesema kuwa viwanja hivyo vianze kuuzwa mara moja kuanzia wiki ijayo ambapo wananchi waliovamia kwa miaka mingi na wapo kwenye eneo hilo watauziwa kwa gharama ya shilingi 3,000 kwa mita ya mraba wakati wengine watakaohitaji viwanja watauziwa kwa shilingi 15,000, 17,000 na 20,000 kwa mita ya mraba kulingana na matumizi yake kama makazi biashara au matumizi mengine.

Vilevile RC Chalamila amewaeleza wananchi wa eneo hilo na ambao watanunua viwanja kuwa Rais Dk. Samia ameshapeleka huduma muhimu za kijamii kwenye eneo hilo ikiwemo umeme na maji na kwamba barabara ipo kwenye mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami kupitia TANROAD

Kwa upande wa Afisa mipango miji Manispaa ya Kinondoni Arkadius Haule amewahakikishia wananchi kuwa viwanja hivyo vyote vimepimwa na vitauzwa kwa kuzingatia uhitaji wa mnunuzi huku Ali Mirambo Meneja Mkuu wa DDC akiwahakikishia wananchi kuwa eneo hilo ni mali ya shirika hilo hivyo wanauziwa na mmiliki halisi

Leave a Reply